24 April 2012

Yanga SC yamng'ang'ania Papic

Na Elizabeth Mayemba

UONGOZI wa Klabu ya Yanga umesema Kocha Mkuu wa timu hiyo, Kostadin Papic bado ni kocha wao halali kwa kuwa mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu huu.

Jana Papic alikaririwa na vyombo vya habari akidai kwamba leo ndiyo mwisho wa mkataba wake wa kuinoa timu hiyo, ambapo pia aliwaaga mashabiki wa timu hiyo, mara baada ya timu yake na Polisi Dodoma kucheza katika mechi waliyoshinda mabao 3-1.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Selestine Mwesiga alisema Papic mkataba wake unaishia mwisho wa msimu ambapo pia alitumia nafasi hiyo kuwaonesha waandishi wa habari mkataba wa kocha huyo, ambao unaonesha unamalizika mwisho wa msimu huu wa 2011/2012.

"Papic ni kocha wetu halali na anatambulika kisheria, hivyo akiondoka kabla ya msimu kumalizika hiyo ni kesi nyingine, kwani hata akimaliza mkataba wake uongozi unaweza kukaa naye tena na kufanya naye mazungumzo mapya, tunaamini Papic ni mwelewa hatatufanyia uhuni wowote," alisema Mwegiga.

Alisema hakuna kocha ambaye anafanya kazi zake kwa uhuru kama Papic, kwani hata siku moja hakuna kiongozi ambaye aliwahi kumpangia timu katika mechi yoyote ile, hata wachezaji wanaposafiri nje ya nchi au nje ya Dar es Salaam ni yeye ambaye huwa anapanga timu.

Akizungumzia mshahara wa kocha huyo, ambaye amelalamika kwamba hajalipwa miezi miwili, Mwesiga alisema Papic anadai mshahara wa mwezi wa tatu ambao nao ameshaupunguza.

"Papic mshahara wake kwa mwezi ni sh.11,270,000 na Februari kachukua wote, hivyo umebaki wa mwezi wa tatu ambao nao ameupunguza, anavyolalamika kwamba anadai miezi miwili tunamshangaa, kwani hata mwezi huu bado haujamalizika," alisema.

Kwa mujibu wa Papic alisema anatarajia kuondoka nchini Aprili 26, mwaka huu na pia yupo katika mipango ya kuzungumza na mwanasheria wake ili aweze kuishitaki Yanga Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), kwa kutolipwa mshahara wa miezi miwili.

No comments:

Post a Comment