RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amesema kama angekuwa yeye ni kamati angetoa adhabu kali kwa wachezaji wa Yanga kutokana na vitendo vya utovu wa nidhamu walivyofanya wakati wa mechi yao dhidi ya Azam FC.
Wachezaji wa Yanga, Nurdin Bakari, Stephano Mwasika, Omega Seme, Nadir Haroub 'Canavaro' na Jeryson Tegete katika mechi hiyo iliyochezwa Machi 10, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam walimpiga mwamuzi Israel Nkongo na baadaye Kamati ya Ligi iliwapa adhabu tofauti tofauti.
Kauli hiyo ya Tenga aliitoa juzi wakati wa ufungaji wa Mkutano Mkuu wa TFF, baada ya Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya timu hiyo ambaye pia ni mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF akiwakilisha klabu za Mkoa wa Dar es Salaam, Mohamed Bhinda kumuomba rais huyo awaombee msamaha wa adhabu ya kulipa faini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura ilimnukuu Tenga akisema: "Namshukuru Bhinda kwa ujasiri alioonesha wa kuomba radhi mbele ya wajumbe hawa kwa kitendo kile, kuwa mimi ni muumini wa kanuni na adhabu hizo zimetolewa kwa mujibu wa kanuni, siwezi kutoa msamaha, hivyo wachezaji hao walipe faini hizo.
Taarifa hiyo ilieleza, Rais Tenga hawezi kuziingilia Kamati za TFF katika uamuzi kwani zina watu waadilifu na angekuwa yeye binafsi ndiyo anayetoa adhabu, angetoa adhabu kali zaidi kwa vile vitendo vya kupiga waamuzi havikubaliki katika mchezo wa mpira wa miguu.
Kabla ya Tenga kuzungumza hivyo, Bhinda aliwaomba radhi Wajumbe wa mkutano huo kwa kitendo cha wachezaji wao, kumpiga mwamuzi na ndipo baadaye alipomuomba Tenga awaombee msamaha kutokana na kitendo hicho.
Mkutano huo wa kila mwaka ulifanyika kwa siku mbili kati ya Aprili 21 na 22 mwaka huu kwenye Ukumbi wa NSSF Waterfront, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wajumbe 104 ambapo mkutano ulipokea taarifa, kufanya uamuzi katika masuala mbalimbali na mengine yaliyojitokeza.
No comments:
Post a Comment