24 April 2012

Simba yaendeleza wimbi la ushindi

:: Mechi ya Azam, Mtibwa Utata
Na Elizabeth Mayemba

VINARA wa Ligi Kuu Bara, Simba jana waliendeleza kimbunga cha ushindi baada kuishindia Moro United mabao 3-0 katika ya ligi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kwa ushindi huo Simba ambao wana pointi 59 wakifuatiwa na Azam sasa wanahitaji pointi ili waweze kutangazwa kuwa mabingwa wapya wa Tanzania Bara.


Simba ilianza kupata bao la kwanza dakika ya 10 kwa mkwaju wa penalti uliokwamishwa wavuni na Patrick Mafisango, baada ya beki wa Moro United kuunawa mpira wakati akiwa katika harakati za kuokoa hatari langoni mwake.

Awali Uhuru Selemani aliikosesha Simba bao la wazi dakika ya sita, baada ya kumegewa pande murua na Emmanuel Okwi.

Ikicheza ikiwa na uchu wa mabao Simba iliongeza bao la pili dakika ya 33, kupitia kwa Haruna Moshi 'Boban' baada ya kuinasa pasi ya Uhuru.

Dakika ya 36 Okwi, alikosa bao akiwa na yeye na kipa wa Moro United baada ya kupaisha mpira juu ya lango.

Baada ya kushambuliwa mfululizo, Moro United ilizinduka dakika tano za mwisho wa kipindi cha kwanza kufanya mashambulizi mfululizo, lakini hata hivyo mabeki wa Simba walikaa imara kuondoa hatari langoni mwao.

Kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko ambapo Simba iliwatoa Shomari Kapombe, Gervas Kago na Uhuru wakaingia Felix Sunzu, Salum Machaku na Said Nassor 'Cholo'.

Moro United nayo iliwatoa Benedict Ngassa na Hilal Bingwa na wakaingia Kelvn Charles na Simon Msuva.

Mabadiliko hayo yaliisaidia zaidi Simba, ambayo iliandika bao la tatu dakika ya 73 lililowekwa wavuni na Sunzu, ambaye aliunganisha krosi ya Okwi.

Naye Specioza Joseph anaripoti kuwa mechi nyingine ya Ligi Kuu iliyochezwa Uwanja wa Chamazi nje kidogo ya Dar es Salaam huku ilimalizika kwa utata baada ya Mtibwa kukataa penalti waliyopewa Azam dakika ya 88 huku timu hizo zikiwa zimefungana bao 1-1.

Wachezaji hao waligoma, baada ya mwamuzi Rashid Msangi kutoa penalti hiyo dakika 88 wakidai kuwa si halali hivyo hatima ya mchezo huo itasubiri ripoti ya Kamisaa na uamuzi wa Kamati ya Ligi.

Azam ndiyo ilianza kupata bao dakika ya kwanza lililowekwa kimiani na Mrisho Ngassa, ambaye aliwazidi mbio kipa wa Mtibwa Sugar Deogratius Munishi pamoja na mabeki wake.

Dakika ya 18 Mtibwa Sugar ilisawazisha bao hilo kupitia kwa Salum Swed, ambaye alipiga shuti la adhabu na mpira kugonga mwamba na kisha kutinga wavuni.

Adhabu hiyo ilitolewa na mwamuzi wa mechi hiyo baada ya beki wa Azam, Said Morad kumchezea rafu mshambuliaji wa Mtibwa Said Bahanuzi.

Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kushambuliana kwa zamu, huku Bahanuzi akitolewa nje kwa kadi nyekundu na mwamuzi Rashid Msangi wa Mpwapwa baada ya kumfanyia madhambi, Salum Abubakari 'Sure Boy'.

Katika kipindi hicho Azam FC ilifanya mabadiliko kwa kumtoa Jabir Aziz na kumwingiza Abdi Kassim 'Babi'.

Mtibwa Sugar ilipata bao dakika ya 62, lakini hata hivyo lilikataliwa na mwamuzi baada ya kipa wa Mwadini Ali kutema mpira ambao ulijazwa wavuni na Awadh Juma.

Kukataliwa kwa bao hilo kuliwafanya wachezaji wa Mtibwa kumlalamikia mwamuzi huyo kwa kulikataa goli hilo.

Hata hivyo dakika ya 87, Azam walipata penalti baada ya beki mmoja kuunawa mpira katika eneo la hatari, lakini wachezaji wa Mtibwa waliigomea kwa madai kuwa si halali.

Baada ya wachezaji hao kuigomea penalti hiyo mwamuzi alisubiri kwa dakika tatu na kupuliza filimbi ya kumaliza mpira

No comments:

Post a Comment