17 April 2012

Wakulima wadogo wadogo kutoa tamko leo

Na Lilian Justice, Morogoro
MTANDAO wa Vikundi vya Wakulima Wadogo Tanzania (MVIWATA) umeandaa kongamano la kitaifa ambalo pamoja na mambo mengine litajadili na kutoa tamko la kupinga mauaji ya wakulima wadogo nchini hasa wanaouawa katika harakati za kutetea ardhi yao.
Aidha, kongamano hilo
linatarajiwa kufanyika mjini
Morogoro leo ikiwa ni sehemu ya
maadhimisho ya siku ya Wakulima
Wadogo Ulimwenguni ili kujadili
athari za uporaji wa ardhi kwa
wazalishaji wadogo nchini.
Hayo yalibainishwa jana mkoani
Morogoro na Mratibu Mkuu wa
Maandalizi ya Kongamano hilo Bw.
Thomas Laiser.
Alisema kuwa, MVIWATA
imeandaa kongamano hilo ili
kuzungumzia mustakabali mzima
wa wakulima wadogo Tanzania,
ikiwemo mauaji ya wakulima
yanayoendelea kutokea wakati wa
harakati za kuwaondoa kwenye
maeneo yao.
Katika miaka ya hivi karibuni
nchini Tanzania, tumeshuhudia kasi
ya uporaji wa ardhi ya wazalishaji
wadogo vijijini, ikijumuisha
matumizi ya nguvu kupita kiasi na
hata mauaji jambo ambalo halitoi
ishara njema ya hatma ya wakulima
na wazalishaji wengine wadogo,
alisema Bw. Laiser ambaye pia
ni Ofisa Ushawishi na Utetezi wa
MVIWATA.
Aidha Bw. Laiser alisema kuwa
uhamishwaji kwa nguvu ili kupisha
wawekezaji wa ndani na nje na
wakati mwingine upanuzi wa ardhi
za hifadhi, zimetajwa kuwa sababu
za kuhalalisha vitendo hivyo
ambavyo vimewaacha wazalishaji
wengi wadogo katika baadhi ya
maeneo wakiwa wamepoteza
makazi, mali na maisha yao.
Pia akitolea mfano wa matukio ya
kuwahamishwa kwa nguvu wafugaji
katika Bonde la Ihefu, Hifadhi
ya Loliondo, Malinyi Ulanga,
Meatu, Kiteto na kwingineko nchini
yakiwemo mauaji ya wakulima
watano wilayani Ulanga siku za
hivi karibuni alisema ni mfano wa
adha ambazo wazalishaji wadogo
wamekuwa wakikabiliana nazo
kutokana na uporaji wa ardhi
unaoendelea kufanyika.
“Kwa sababu hizo basi
Mtandao wa Vikundi vya Wakulima
Wadogo nchini unaungana na
wanaharakati wengine nchini na
ulimwenguni kuwaleta pamoja
wakulima ili waweze kujadili na
kupaza sauti yao iweze kusikika
na watunga sera na watoa maamuzi
nchini ili kuzuia kuendelea kwa
uporaji huo wa raslimali ardhi
ambayo wanaitegemea kwa
uzalishaji na ustawi wa maisha
yao," alisema Bw. Laiser.
Alisema, kongamano hilo
pia litaweza kujadili athari
zinazowakabili wanawake na
watoto vijijini katika harakati za
utwaaji ardhi na kutoa mwito kwa
viongozi wa kisiasa na serikali
wa ngazi mbalimbali kuwalinda
na kuisimamia haki ya ardhi ya
wazalishaji wadogo vijijini.
Bw. Laiser alisema kongamano
hilo litakuwa na washiriki zaidi ya
90 wakiwemo wakulima 70 kutoka
mikoa mbalimbali ya Tanzania
kati yao theluthi mbili wakiwa ni
wanawake.
"Washiriki wengine kwenye
kongamano hilo watakuwa ni
wanahabari, waalikwa toka
mashirika yanayotetea haki za
ardhi nchini, wawakilishi wa taasisi
zingine za kiraia, wanaharakati,
wanataaluma na baadhi ya viongozi
na wafanyakazi wa MVIWATA,"
aliongeza.
Hata hivyo alisema kuwa
maadhimisho hayo ambayo
huadhimishwa kila ifikapo Aprili 17
kila mwaka ni siku ya maadhimisho
ya harakati za wakulima wadogo
ulimwenguni (International Day of
Peasants Struggle).
Maadhimisho hayo hufanyika
ikiwa ni kumbukumbu ya mauaji ya
wakulima wadogo 19 yaliyotokea
nchini Brazil mwaka 1996 wakiwa
katika harakati za kutetea haki
yao na kuzuia uporaji wa ardhi
waliyokuwa wakiitegemea kwa
uzalishaji.

No comments:

Post a Comment