17 April 2012

Udanganyifu udahili wanafunzi wapata mwarobaini

TANZANIA ni moja ya nchi inayofanya kila jitihada kuinua kiwango cha elimu ili kuleta maendeleo lakini
pia serikali imeweka mkakati wa kuona kila Mtanzania anakuwa na elimu angalau ya kidato cha nne.
Wakati serikali ikiweka mkazo
kuinua na kuboresha kiwango cha
elimu kwa upande mwingine wadau
wa elimu wamekuwa wakilalamikia
suala la elimu huku baadhi ya taasisi
zikilaumiwa kushindwa kusimamia
vema tasnia hiyo nchini.
Wamekuwa wakionyesha kukerwa
na taasisi mbalimbali zinazosimamia
suala zima la elimu nchini kutokana
na uzembe unaojitokeza.
Wakati Tume ya Elimu ya Vyuo
Vikuu (TCU) ikipewa jukumu la
kusimamia suala zima la uboreshaji
wa elimu kwa kuwapangia wanafunzi
vyuo na masomo yao, imeonyesha
kuwa taasisi zingine zimekuwa
zikishindwa kutoa ushirikiano na
kusababisha kuwepo kwa udanganyifu
mkubwa katika kipindi cha udahili wa
wanafunzi wanaokwenda vyuoni kwa
wakati ule.
TCU inaweza kufanya kazi zake
vizuri na hasa katika kuhakikisha
kila mwanafunzi anakuwa na sifa za
kuingia chuoni lakini kutokana na
baadhi ya wanafunzi kupata nafasi
hizo bila kupitia kwa chombo hicho
imekuwa changamoto kwa taasisi
hiyo.
Mbali na TCU kuonyesha
makali ya kutaka kuhakikisha kila
mwanafunzi anachaguliwa nao,
baadhi ya taasisi za elimu NECTA
na NACTE zimeshindwa kudhibiti
mianya mbalimbali ya wanafunzi
kujipenyeza mpaka kupata nafasi za
kuingia vyuoni.
Ikumbukwe kuwa, kazi kubwa ya
tume hiyo ni kusimamia udahili wa
wanafunzi wanaoingia elimu ya juu
yaani vyuo vikuu katika kuhakikisha
kuwa kila mtu anakuwa na sifa ya
kuingia huko akiwa na vielelezo
vilivyokamilika.
Jitihada hizo zimekuwa zikipata
doa baada ya kuwa na maswali mengi
kwa wadau kuhoji wanafunzi kuingia
vyuoni bila kuwa na sifa madhubuti
Katika hatua nyingine TCU pia,
wamekuwa wakionyesha programu
mbalimbali ambazo mwanafunzi
anayeingia chuoni kuweza kujua
anakwenda kusoma nini.
Katika hilo hivi karibuni TCU
imezindua toleo la pili la mfumo wa
udahili wa pamoja wa vyuo vya elimu
ya juu nchini.
Katika toleo hilo Bw. Sifuni
Mchome ambaye ni Katibu Mtendaji
wa TCU anasema, toleo hilo litasaidia
kutatua changamoto walizokuwa
wakikabiliana nazo katika nyanja ya
elimu ya juu.
Anasema, kazi kubwa ni kuhakikisha
wanafunzi wanaodahiliwa wanakuwa
na sifa za kuingia chuo kikuu kutokana
na udanganyifu uliojitokeza hivi
karibuni kwa wanafunzi kuingia huko
bila kuwa na sifa stahiki.
"Nadhani toleo hili litasidiwa kwa
kiwango kikubwa kutatua kero na
changamoto mbalimbali kutoka
kwa wanafunzi hao," anasema.
Wakati Tume ikipanga kutatua
changamoto hizo hivi karibuni
Naibu Waziri wa Elimu ya Ufundi
na Mafunzo Bw. Philipo Mulugo
ameoneshwa kukerwa na NECTA
na NACTE kushindwa kusimamia
majukumu yake kikamilifu.
Anasema, vyombo hivyo
vimekuwa vikiruhusu wanafunzi
wasio na vigezo kuingia vyuo vya
elimu ya juu kwa kutosimamia
wanafunzi kughushi vyeti.
Bw. Mulugo anasema, mbali na
vyombo hivyo lakini pia wakuu wa
shule mbalimbali nchini wamekuwa
wakichangia kwa kiasi kikubwa
kuingiza wanafunzi wasio na vigezo
vya kuchaguliwa na kuwapeleka
vyuo vikuu.
"Rushwa inatawala mno katika
nyanja hizi na ndiyo maana
inapelekea kushindwa kupata
wataalamu, imekuwa kama kawaida
kwa walimu na vyombo mbalimbali
vya elimu kitu ambacho kitarudisha
nyuma maendeleo ya elimu nchini,"
anasema Bw. Mulugo
Anasema NACTE na NECTA
wanafahamu kuwa katika vyuo
kuna baadhi ya wanafunzi ambao
hawana sifa hatua ambayo ni hatari
kwa taifa siku za baadaye.
Bw. Mulugu alitoa mfano wa
Kigoma ambapo, wanafunzi 300
wasio na vigezo walipewa nafasi
ya kujiunga na elimu ya juu bila ya
kuwa na sifa stahili.
Serikali haitavumilia kuona
wanafunzi wasio na vigezo
wakijiunga na elimu ya juu kwa
kutoa rushwa huku walengwa
wakikosa nafasi.
Katika hatua nyingine Bw.
Mulugo anakerwa na utitiri wa
vyuo jijini Dar es salaam ambavyo
havina sifa za kutoa elimu ya juu na
kujenga hatari ya kudidimiza elimu
hiyo nchini.
Katika hilo anashauri kuwa,
wanafunzi waache kukimbilia vyuo
hivyo ambavyo havina sifa badala
yake waende kwenye vyuo ambavyo
vimepata usajiri nakutambuliwa na
TCU.
Anasema, mfumo wa udahili
wa wanafunzi vyuoni utasaidia
kubaini wanafunzi wenye vyeti feki
na chuo ambacho hakijasajiliwa
ambao wana lengo la kuendelea na
elimu ya juu. Katika hatua hiyo ni
dhahili wadau mbalimbali nchini
kushirikiana na TCU ili kuboresha
elimu ya juu katika Taifa.
Pia, ni vema walimu wakawa
waaminifu katika kuhakikisha
mtu anakuwa na stahili ya kwenda
kusoma elimu hiyo huku akiongozwa
na sifa alizokuwa nazo ili kupata
wataalamu wenye vigezo.
Hata hivyo tunaishauri TCU
kufanya kazi zake kwa kufuata
taratibu zilizopo lakini pia
kuendelea kuelekeza kile ambacho
kinaweza kuwasaidia Watanzania
hasa wanafunzi katika kupata elimu
ya juu.

No comments:

Post a Comment