17 April 2012

Uamuzi wa serikali kuipa meno SSRA wapongezwa

Na Rose Itono
BAADHI ya wadau wa masuala ya Hifadhi ya Jamii nchini, wameipongeza Serikali kwa kupitisha muswada wa marekebisho ya sheria za mifuko ili kuiwezesha Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), kufanya kazi zake ipasavyo.
Wakizungumza na Majira Dar es Salaam jana, baadhi ya wadau hao walisema marekebisho hayo yatawasaidia wananchi wengi.

Bw. Salim Kiluwasha ambaye ni mfanyabiasahara, alisema kwa muda mrefu wanachama wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii wamekuwa hawafaidiki ipasavyo na wengine kuzuiwa kujiunga na mifuko mingine kutokana na sheria zilizopo.

Alisema kupitishwa kwa muswada huo kumefungua njia ya kuwanufaisha wanachama zaidi tofauti na awali.

“Tuna imani kuwa mabadiliko haya ya sheria, yataboresha utendaji wa mifuko hii na kuwafanya wanachama kunufaika zaidi,” alisema.

Mdau mwingine Bw. Santulo Kalago, alisema sheria inayozuia wanachama kujiunga na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii wanayoipenda  ilikuwa kikwazo kwa wananchi wengi.

Alisema wafanyakazi wengi wanapenda kujiunga na mifuko inayofanya vizuri lakini kutokana na sheria kandamizi, walishindwa kufanya hivyo.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Bunge lilipitisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali za zinazohusu sekta ya Hifadhi ya Jamii.

Akiwasilisha Muswada huo, Waziri wa Kazi na Ajira Bi. Gaudencia Kabaka, alisema muswada huo una marekebisho zaidi ya 150 yote yakilenga kubadilisha sheria za mifuko hiyo.

Aliongeza kuwa, lengo la muswada huo ni kuongezea vifungu vya sheria ambavyo havikuwepo. Muswada huo unaruhusu mfanyakazi anayejiunga na ajira kwa mara ya kwanza iwe katika sekta rasmi au isiyo rasmi, kuwa na uhuru wa kuchagua mfuko wa kujiunga nao.

1 comment:

  1. NAOMBA WACHANGIA HOJA NA VIONGOZI WANIJIBU MASWALI YAFUATAYO:

    HII MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII NI MALI YA WANACHAMA WANAOCHANGA HIZO FEDHA AU NI MALI YA SERIKALI? KAMA NI MALI YA WANACHAMA WANAOCHANGIA NI KWA NINI HAWA WANACHAMA WASITHIBITI HII MIFUKO? JE, SERIKALI INACHANGIA HII MIFUKO KWA KIASI GANI ILI IWEZE KUWA NA UMILIKI NA UENDESHAJI WA HII MIFUKO BILA KUWA NA VIONGOZI WAWAKILISHI WALIOCHAGULIWA NA WANACHAMA WANAOCHANGIA? SABABU ZIPI ZINAZOWAFANYA BAADHI YA VIONGOZI WALIOCHAGULIWA NA SERIKALI KWENYE KUNUNUA MAGARI YA KIFAHARI NA KUGAWA MICHANGO YA WANACHAMA KAMA NI FEDHA ZA SERIKALI? MIFUKO HII NI MASHIRIKA YA UMMA? NANI ANARUHUSU FEDHA ZA MIFUKO KAMA YA BIMA YA AFYA KUTOA FEDHA ZA WANACHAMA KUJENGA HOSPITALI NA HUKU WANACHAMA WANAKOSA HUDUMA NA DAWA? NI SABABU ZIPI ZINAZOYAFANYA MASHIRIKA KAMA PPF KUJENGA MAJENGO KAMA UDOM? HAYA MASHIRIKA NI VYOMBO VYA FEDHA VYA KUGAWA MIKOPO NA UWEKEZAJI? KAMA NI HIVI BENKI YA RASLIMALI (TIB) NA BENKI NYINGINE NCHINI ZITAFANYA KAZI GANI AU KAZI YA TIB NI KUGAWA PEMBEJEO BADALA YA KSAIDIA WAWEKEZAJI WADOGO?

    ReplyDelete