17 April 2012

Wabunge CHADEMA tumieni busara, ushiriki wenu EALA ni muhimu

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), jana kilitangaza kujitoa katika uchaguzi wa wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki ambao unafanyika leo.
Msimamo wa chama hicho kujitoa katika uchaguzi huo, ulitangazwa jana na mjini Dodoma na Mwenyekiti CHADEMA Taifa na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bw. Freeman Mbowe.

Katika maelezo yake kwa waandishi wa habari, Bw. Mbowe alisema mchakato wa uchaguzi huo una kasoro mbalimbali pamoja na malalamiko yao kutosikilizwa na Serikali.

Alisema uchaguzi huo ulipaswa kufanyika kwa mujibu wa ibara ya 50 ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Kanuni ya Bunge ya 12 ya Bunge la Tanzania lakini kumeku na ukiukwaji mkubwa wa kanuni.

Bw. Mbowe aliongeza kuwa, mchakato wa uchaguzi huo pia umetawaliwa na rushwa inayotolewa na baaadhi ya wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Aliongeza kuwa, pamoja na chama hicho kulalamikia hali hiyo kwa Serikali na Bunge, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa hivyo wao kama chama makini, hawawezi kushiriki uchaguzi huo.


Sisi tunasema kuwa, pamoja na CHADEMA kulalamikia hali hiyo, ushiriki wenu katika uchaguzi huo ni muhimu ili kusimamia na kulinda haki za Watanzania pamoja na rasilimali za Taifa.

Pamoja na Serikali kupuuza hoja zenu kama mnavyodai, bado mnanafasi ya kushiriki uchaguzi na kufanya vizuri kama ilivyotokea katika chaguzi mbalimbali ambazo nyingi zinatawaliwa na mizengwe.

Imani yetu ni kwamba, msimamo mlioutoa jana mtaufikiria mara mbili ili kutetea maslahi ya Watanzania wanyonge na kulinda rasilimali za nchi ili kukuza uchumi na kuharakisha maendeleo.

Historia inaonesha kuwa, kawaida ya chaguzi mbalimbali hasa za kisiasa, suala la mizengwe ni jambo la kawaida hivyo jambo la msingi ni kuonesha ukomavu wenu kisiasa.

Choche CHADEMA, rudini katika uchaguzi kwani uwakilishi wenu ni fursa nzuri ya kukitangaza chama chetu kwa kuonesha uwezo wa kujenga hoja mbalimbali ambazo zitakuwa zikijadiliwa katika bunge hilo.

No comments:

Post a Comment