03 April 2012

Poulsen kumrudisha Bocco Taifa Stars

Na Zahoro Mlanzi
SIKU chache baada ya mshambuliaji wa timu ya taifa (Taifa Stars) na Azam FC, kuandika barua ya kustaafu kucheza timu ya taifa, Sekretarieti ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imeibuka na kusema hatma yake ipo mikononi mwa kocha wake, Jan Poulsen.
Bocco alifikia uamuzi huo, baada ya kuzomewa mfululizo na mashabiki wa soka wakati akiichezea timu ya taifa, ambapo kwa kufanya hivyo anaamini ataepukana na shida anazozipata kutoka kwa mashabiki wa timu hiyo ya taifa.

Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema sekretarieti yao imepokea barua hiyo na kuijadili na kuamua kuipeleka kwa kocha Poulsen, ambaye yeye ndiye mwenye mamlaka ya kuamua hatma ya mshambuliaji huyo.

"Unajua katika soka la sasa, kocha ndiye anayechagua wachezaji na yeye ndiye anayemjua vizuri Bocco, kwa kuwa hukaa naye kambini muda mwingi, hivyo tutamfikishia barua na atajua nini cha kufanya katika hilo.

"Tunatarajia Poulsen atakaa na Bocco kuzungumzia hilo pamoja na kumshauri, kwani hata wao TFF wanasikitishwa na uamuzi huo licha ya kwamba huwa anapata wakati mgumu anapokuwa uwanjani kwa kuzomewa," alisema.

Akizungumzia suala la kuzomea kwa undani, Wambura alisema hilo lipo sehemu yoyote na hata katika nchi zilizoendelea ila suluhisho la hilo ni kuongeza bidii na kufunga, ili kuwakata mdomo wanaozomea.

"Mfano mzuri nahodha wa Yanga katika mechi yao na Coastal, alizomewa muda wote lakini aliwaonesha ishara ya kwamba watulie timu yake itafanya vizuri na hilo mwisho wa siku lilifanikiwa," alisema.

Alisema wanakiri kitendo kinachofanywa na mashabiki si cha kiungwana, kwani kitendo hicho kinapaswa kufanywa na mashabiki wa timu pinzani, lakini suala hilo lipo nje ya uwezo wao ila wataendelea kutoa elimu.

No comments:

Post a Comment