02 April 2012

Mkwassa ataka Twiga Stars iweke kambi mapema

Na Amina Athumani
KOCHA Mkuu wa timu ya soka la Wanawake (Twiga Stars), Charles Boniface Mkwasa amelitaka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kuiweka kambini mapema timu hiyo mara kambi hiyo itakapovunjwa keshokutwa kwa ajili ya kujiandaa na kambi ya raundi ya pili.
Twiga Stars ipo kambini mkoani Pwani tangu Machi 25, mwaka huu ikijiandaa kutafuta tiketi ya kucheza Fainali za Nane za Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) zitakazofanyika Novemba, mwaka huu  Equatorial Guinea.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkwasa alisema kambi hiyo inatarajiwa kuvunjwa Jumatano ambapo wataisubiri TFF iwape tena tarehe ya kuendelea na kambi hiyo katika raundi ya pili.

Alisema kutokana na hali hiyo ni vema TFF wasichelewe kuwaweka kambini kwa kuwa hakuna ligi endelevu ya wanawake itakayowafanya vipaji vyao kuendelea kukomaa.

"Unapovunja kambi halafu wachezaji wakikaa nyumbani bila mashindano wala mazoezi ya mara kwa mara watakapoitwa tena kambini ni sawa na kuanza moja, hivyo tunashauri mara baada ya kambi hii kuvunjwa basi wachezaji wasiwekwe muda mrefu bila kuitwa kambini,"alisema Mkwasa.

Alisema Twiga Stars inahitaji nguvu ya ziada  na mazoezi ya kutosha ili kuboresha uwezo wao waliouonesha katika mechi yao dhidi ya Namibia ili kuiondosha pia Ethiopia katika mechi ya kwanza itakayofanyika Mei 26, mwaka huu jijini Addis Ababa.

No comments:

Post a Comment