*Tume ya Haki za Binadamu yashauri washtakiwe
*Yaeleza sababu ya kukaa kimya wakati wa mgomo
*Yasisitiza madaktari walivunja matakwa ya katiba
Na Grace Ndossa
TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, imesema madaktari walioshiriki kwenye mgomo na kusababisha huduma za matibabu kusuasua, wanapaswa kushtakiwe mahakamani.
Mkurugenzi wa tume hiyo, Bw. Francis Nzuki aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na Majira baada ya kumalizika kwa mkutano wa wadau wa haki za binadamu.
Pamoja na mambo mengine, mkutano huo ulijadili mpango wa dunia na wajibu wa mitandao ya kijamii kulinda na kuhamasisha haki za binadamu.
Alisema madaktari hao walikiuka haki za binadamu na kuwanyima haki ya kuishi watu waliopoteza maisha kwa sababu ya kukosa matibabu kutokana na mgomo huo.
Bw. Nzuki alisema, katika kipindi chote cha mgomo tume hiyo ilikaa kimya bila kutoa tamko kutokana na ukweli kwamba, kabla madaktari hawajafanya mgomo walikuwa wakifahamu athari zinazoweza kutokea.
“Kabla hawajagoma walikuwa wakijua kufanya hivyo ni kukiuka haki za binadamu na kuwanyima watu haki ya kuishi kama ilivyoainishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema Bw. Nzuki.
Aliongeza kuwa, kipindi cha mgomo huo maofisa wa tume hiyo walitembelea Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kujionea haki ya kuishi ilivyokuwa ikikiukwa na madaktari hao.
Katika kipindi hicho, Majira lilibahatika kukutana na baadhi ya maofisa wa tume hiyo katika hospitali hiyo ambao walisema lengo la kutembelea MNH ni kujionea haki ya kuishi imekiukwa kwa kiwango gani kwa watu wasio na hatia.
“Tupo hapa kuangalia athari zilizotokana na mgomo ili baadae tuweze kutoa tamko letu,” walisema maofisa hao walipokutana na waandishi wetu kipindi cha mgomo.
Awali Bw. Nzuki alisema hivi sasa jamii kubwa inaweza kuwasiliana kutokana na ongezeko la mitandao ya kijamii.
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam kutoka Shule ya Sheria, Profesa James Jesse, alisema mkutano huo utajadili mpango kazi wa tume ambao utakuwa unatumika kuainisha haki za binadamu na utawala bora.
Alisema mpango kazi huo umelenga katika maeneo 24 na umegawanyika kwenye makundi makuu manne.
Kundi la kwanza linalenga haki za kiraia na kisiasa, haki ya kuishi na kupata haki ya msingi mahakamani. Kundi jingine linahusu haki za kijamii na kiuchumi ambazo kwenye katiba hazitambuliki, haki ya kupata elimu, afya bora na ulinzi ili mtu anapopata majanga au kufukuzwa kazi kundi hilo liwe limeainishwa.
Alisema mpango huo unatarajiwa kukamilika Juni mwaka huu na kupelekwa katika Baraza la Mawaziri ili kupata baraka ili uweze kuzinduliwa.
ninahisi kuna tatizo katika bongo zetu, ni yupi anapaswa kushitakiwa mwenye hospitali au raia kwa raia wanaosaidiana wao kwa wao?
ReplyDeleteSawa Bw. Msses. Serikali ipelekwe mahakamani. Tume ya haki ichunguze ukweli uko wapi.
DeleteTume inanyamza inapoona wagonjwa wanakufa kwa kukosa dawa kulazwa chini, madawa, vifaa na mali kuibwa, fedha kufujwa na hizo hospitali. Iwaunge mkono Madaktari.
Tume hiyo ingefanyakazi ya kuihimiza serikali kushughulikia madai ya madaktari siyo kufanyakazi ya kuwagombanisha madaktari na serikali.Kwanza hiyo tume inatetea haki gani za raia?ni haki ngapi za raia zinavunjwa wakati ipo?
ReplyDelete