05 April 2012

Adhabu za Yanga zaitoa 'kamasi' TFF

Na Zahoro Mlanzi
KIKAO cha Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kimeshindwa kumalizika juzi kama ilivyotarajiwa kutokana na wajumbe waliohudhuria kikao hicho, baada ya kutokea mvutano katika kufikia muafaka wa rufani zilizowasilishwa na Klabu ya Yanga.
Kikao hicho kilianza juzi jioni na kuendelea tena jana chini ya Mwenyekiti wake Kamanda Mstaafu wa Polisi, Alfred Tibaigana akiwa na baadhi ya wajumbe wake pamoja na viongozi wa Yanga, wajumbe wa Kamati ya Ligi na wawakilishi wa TFF.

Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana baada ya kuulizwa kilichofikiwa katika kikao cha kamati hiyo iliyokutana juzi, Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Boniface Wambura alisema kikao kilishindwa kumalizika na kwamba kilitarajiwa kumalizika jana usiku.

"Kwa kweli hatutaweza kutoa taarifa juu ya kilichoamuliwa katika kikao hicho kama nilivyoahidi kutokana na kuwa hakikumalizika, hivyo kinaendelea leo (jana) jioni na kwamba watakalofikia lolote kesho (leo) au keshokutwa tutatoa taarifa," alisema Wambura.

Kikubwa katika rufani hiyo, Yanga walipinga adhabu iliyotolewa na Kamati ya Ligi ya kuwafungia wachezaji wao watano, pamoja na kupinga maamuzi yaliyotolewa na mwamuzi Israel Nkongo, katika mechi yao hiyo dhidi ya Azam FC.

Wachezaji waliofungiwa ni Stephano Mwasika aliyefungiwa mwaka mmoja na faini ya sh. milioni moja, Jerry Tegete kifungo cha miezi sita na faini ya sh. 500,000, Nadir Haroub 'Cannavaro' alifungiwa mechi sita na faini ya sh. 500,000, Omega Seme na Nurdin Bakari wao walifungiwa mechi tatu kila mmoja.

Kutokana na adhabu hiyo, Yanga ilikata rufani kwa Kamati ya Tibaigana ambapo baada ya kamati hiyo kuomba vielelezo kwa kamati husika na kukosekana iliamua kuzisimamisha kwa siku 14 kutoa nafasi ili kupata ushahidi wa kutosha isipokuwa kwa zile zilizotolewa ndani ya dakika 90 ya mchezo.

Wakati hilo, likiwa bado halijapatiwa ufumbuzi kamati ya ligi ikaipoka Yanga pointi tatu na kuipa Coastal Union ya Tanga, pamoja na mabao mawili kutokana na kumchezesha Canavaro ikidaiwa hajamaliza adhabu aliyotakiwa kuitumikia ya kukosa mechi tatu kitu ambacho kimeibua mjadala mwingine upya.

Katika hatua nyingine, alipotafutwa Ofisa habari wa Yanga, Louis Sendeu kuthibitisha kwamba wamekata rufani juu ya kupokwa pointi, alisema wanasubiri kwanza maamuzi ya Kamati ya Nidhani, ndipo watajua la kufanya.

Hata hivyo wakati gazeti hili linakwenda mitamboni, zilipatikana taarifa kwamba katika hicho cha Kamati ya Nidhamu kulikuwa na mvutano mkubwa huku Kamati ya Ligi ikionekana kuzidiwa hoja na wajumbe wengine juu ya adhabu walizotoa kwa wachezaji wa Yanga.

No comments:

Post a Comment