16 April 2012

CHADEMA wakosoa utendaji wa polisi

*Wadai wakitumika kisiasa, amani iliyopo itapotea
Na Suleiman Abeid, Shinyanga
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimelitaka Jeshi la Polisi nchini kufanya kazi kwa kuzingatia sheria za nchi badala ya kutumika kisiasa zaidi.

Katibu Mkuu wa chama hicho Taifa, Dkt. Wilbroad Slaa, aliyasema hayo juzi wakati akihutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Shinyanga katika Viwanja vya Shycom.

Alisema polisi wanapaswa kufahamu jukumu walilonalo ambalo ni kudumisha amani na utulivu nchini na kutekeleza wajibu huo kwa kuzingatuia sheria na taratibu.

Aliongeza kuwa, kama polisi watakubali kutumika kisiasa kusahau maadili ya kazi yao amani na utulivu uliopo utatoweka na wao ndiyo watakuwa chanzo cha kutokea machafuko ya kisiasa nchini.

Kauli Dkt. Slaa, ilitokana na majibu ya Jeshi la Polisi wilayani Shinyanga yaliyopelekwa kwa uongozi wa CHADEMA Mkoa kuhusu mkutano uliohutubiwa na kiongozi huyo.

Alisema chama chochote cha siasa kinapokuwa na mkutano wa hadhara katika eneo lolote, kinapaswa kutoa taarifa polisi ili waweze kuweka ulinzi katika mkutano na sio kuomba kibali kama majibu ya  OCD yalivyopelekwa kwa uongozi wa CHADEMA.

“Kwa mujibu wa sheria za nchi, polisi hawatoi kibali cha mikutano, wao wanaarifiwa ili watoe ulinzi, kama kuna shughuli yoyote ambayo itasababisha polisi wasiwepo, chama husika huombwa kuahirisha mkutano wake hadi siku nyingine si vinginevyo.

“Barua ya OCD inasema, tunapewa kibali cha kufanya mkutano kwa masharti ya kutotumia maneno yoyote ya uchochezi au kashfa dhidi ya viongozi wa Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM), huu si utaratibu, iweje tupangiwe kitu cha kuzungumza, jukumu lao ni
kutoa ulinzi si kibali wala kupanga nini tuzungumze,”alisema.

Katika hatua nyingine, Dkt. Slaa alisema vyama vyote vya upinzani vilivyoko nchini kazi yao kubwa ni kukikosoa chama kilichopo madarakani au viongozi wake pale wanapokwenda kinyume hivyo kitendo cha polisi kuzuia wasisemwe ni kutaka kuvwanyima uhuru wao kikatiba.

3 comments:

  1. Waeleze hao Maafande wengi bado hawapitia sheria. Pia weledi wao uko chini sanaaaaa. Chadema Hoyee!

    ReplyDelete
  2. Chadema mtachukua nchi,wananchi kuongea kwao ni sanduku la kura tuuuuuuuuuuuuuu.Sisi acha tunyamaze kama wajinga lakini twajua tutafanya nini mwaka 2015 si mbali.Chadema Oyeeeeeeeeeee.
    Dr Slaa unachosema ni sahihi polisi wanaegemea ccm tu hivyo kila raia mwenye akili timamu anajua.Poleni sana ccm.
    Chadema simame imara kwa Yesu aliye Bwana wetu wao ccm wasimame katika nyazifa zao,na wataona mwaka 2015.

    ReplyDelete
  3. Yale yale ya Kikwete kuwapiga watu marufuku wasizungumzie uhai wa muungano. Polisi wanavaa kaptula hawawezi kuwaambia wasomi nini cha kuwaambia wananchi kwenye maswala ya elimu ya uraia. Waache longolongo popi wa Changoja

    ReplyDelete