WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali imesema ufinyu wa bajeti unawafanya washindwe kuwatumia walimu kutoka kisiwani Pemba na maeneo ya mbali kusahihisha mitihani.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Naibu
Waziri wa Wizara hiyo Bi. Zahra Ali Hamad katika Kikao cha Baraza la Wawakilishi wakati akijibu swali la
nyongeza la Mwakilishi wa Jimbo la Mtambwe Bw. Salim Abdalla Hamad (CUF) katika kikao cha baraza hilo kilichoendelea jana mjini hapa.
Bi Hamadi alisema kuwa kwa sasa
wizara imekuwa ikiwatumia walimu
wa Mkoa wa Mjini Magharibi pekee
katika kazi hiyo kutokana na kuwa
walimu hao hawahitaji pesa za
usafiri tofauti na kuwachukuwa
walimu kutoka kisiwani Pemba na
maeneo mengine ya mbali.
Alisema kuwa, katika kufanya
kazi hizo mwalimu wa Pemba pekee
mbali na kugharamiwa mahala
pa kulala na chakula pamoja na
posho pia mwalimu huyo anahitaji
kulipwa sh. 30,000 za mkononi
kila siku ambapo Wizara haina
uwezo huo.
Hivyo alisema kuwa kutokana
na hali hiyo ndio wizara ikaamua
kuwatumia walimu kutoka Mkoa
wa Mjini Magharibi pekee.
Katika swali lake Mwakilishi
huyo alitaka kujua sababu ambazo
zinapelekea walimu wa Pemba
wasishirikishwe katika usahihishaji
wa mitihani.
No comments:
Post a Comment