KAMA tulivyoona katika toleo lililopita kwamba zao la pamba ni moja ya mazao makuu ya kibiashara hapa nchini ambayo huchangia kwa kiasi kikubwa katika pato la Taifa, lakini hata hivyo wakulima wa zao hilo wamekuwa wakilalamika kutosaidiwa na mamlaka zilizokabidhiwa jukumu hilo.
Katika toleo hilo tulieleza suala la utaratibu
wa kilimo cha mkataba ambao umebuniwa
na Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) moja ya
vyombo ambavyo ndivyo vilivyokabidhiwa
jukumu la kumsaidia mkulima.
Pamoja na kubuniwa kwa utaratibu huo,
wakulima wengi wanaupinga wakidai
utasababisha wengi wao kubakia watumwa
au manamba wa kuyatumikia makampuni
watayokuwa wamefunga nayo mikataba ili
kuwezesha kupatiwa pembejeo za kilimo.
Wanachopinga zaidi ni jinsi ya utekelezwaji
wa utaratibu huo ambapo inaonesha
makampuni ndiyo itanufaika zaidi na kilimo
hicho kwa vile hakuna sehemu yoyote ambayo
mkulima anapewa nafasi ya kupanga bei ya
pamba yake.
Chini ya utaratibu huo, kampuni ndiyo yenye
nafasi kutokana na kutakiwa kuwakopesha
wakulima pembejeo ambazo malipo yake
yatakatwa kwenye mauzo mwanya ambao
makampuni hayo yanaweza kutumia na
kumpunja mkulima.
Bodi ya Pamba ambayo ndiyo inayopaswa
kusimamia ustawishaji wa zao la pamba
nchini pamoja na kumsaidia mkulima wa zao
hilo imekuwa ikilaumiwa na wakulima wengi
ambao wanadai imekuwa chanzo kikuu cha
kuporomoka kwa kilimo cha zao hilo katika
maeneo mengi nchini.
Wengi wao wakiwemo wanachama wa
vyama vya ushirika vya msingi wamekuwa
wakidai kwamba bodi hiyo badala ya
kumsaidia mkulima hivi sasa inayakumbatia
makampuni yanayojishughulisha na ununuzi
wa zao hilo kwa kuwapa kila msaada hata
kama msaada huo utakuwa na madhara kwa
mkulima.
Hivi karibuni wakulima hao wamelalamikia
kitendo cha bodi hiyo kuweka sharti gumu
linalowataka wanunuzi wa pamba kulipa kiasi
cha shilingi milioni 50 ili kuweza kuruhusiwa
kununua pamba katika kanda moja ambapo
kwa yule atakayehitaji kununua zaidi ya kanda
moja ni lazima kila kanda ailipie kiasi hicho
cha fedha.
Hali hiyo imesababisha mvutano mkubwa
kati ya wadau wa pamba, vyama vya ushirika
na wakulima wa zao hilo ambapo kwa
upande wa vyama vya ushirika vinadai upo
uwezekano mkubwa vikashindwa kununua
pamba katika msimu wa mwaka huu kutokana
na kutokuwa na uwezo wa kupata kiasi hicho
cha fedha.
Kwa upande wao wakulima wameonesha
wasiwasi kuhusiana na sharti hilo ambapo
wamesema iwapo makampuni mengi
yatashindwa kulipa kiasi hicho cha fedha ni
wazi ni machache tu yenye uwezo wa kifedha
yatakayomudu na hivyo kuondoa kabisa suala
la ushindani katika ununuzi wa zao hilo kwa
msimu wa mwaka huu.
Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima wa
Pamba nchini (TACOGA), Bw. Elias Zizi
anasema, sharti la kuwataka wanunuzi wa
pamba kuchangia kiasi cha shilingi milioni 50
ili kupewa leseni ya kununua pamba ni gumu
na linaweza kusababisha kushuka kwa kiasi
kikubwa kwa bei ya pamba.
Anasema bei ya pamba imekuwa ikiongezeka
zaidi ya bei elekezi inayotangazwa na bodi ya
pamba kutokana na ushindani wa wanunuzi
wanaokuwepo, hivyo iwapo watakuwa
wachache ni wazi mkulima atapunjika.
"Hili ni tatizo, tumeshindwa kuelewana
katika vikao vyetu, sisi kwa upande wetu
tumeamua kwenda kuonana na waziri wa
kilimo, chakula na ushirika aingilie kati suala
hili na kama atashindwa tutakwenda kukutana
na waziri mkuu," anasema Bw. Zizi.
Bw. Shigela Charles mkazi wa kijiji cha
Bunambiyu wilayani Kishapu anasema:
"Sharti hili la bodi ya pamba ni kitanzi kwa
wakulima, wanunuzi wengi uwezo wao
wa kifedha ni mdogo, hivyo watakaomudu
sharti hilo ni wanunuzi wakubwa peke
yao, watakuwa na nafasi ya kupanga bei
wanayoitaka wao."
"Hii hali inatupa wasiwasi wakulima wa
pamba kila mwaka tunakuwa na matatizo
mengi, mwaka jana mwanzoni mwa kilimo
tulisambaziwa mbegu zilizooza, halafu tena
pamba hii chache tunayotarajia kuvuna
huenda ikakosa wanunuzi, tunaomba serikali
itunusuru, ni vyema ikaingilia kati suala hili,"
anasema Bw. Charles.
Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba katika Kanda
ya Ziwa, Bw. Johannes Bwahama anasema,
suala la kutakiwa kampuni ya kununua pamba
kulipia kiasi cha shilingi milioni 50 ili yaweze
kuruhusiwa kununua pamba katika msimu
wa mwaka huu lilikubaliwa katika kikao cha
wadau kilichofanyika hivi karibuni.
Bw. Bwahama anasema, katika kikao
kilichohusisha Chama cha Wafanyabiashara
wa pamba na bodi pia Chama cha wakulima
wa pamba kiliwakilishwa ilikubalika kila
kampuni kulipa sh. milioni 50 kwa kila kanda
itakayofanyia kazi ikiwa ni malipo ya awali
ya pembejeo watakazopatiwa.
Anasema, wanaopinga utaratibu huu si
wakulima halisi wa zao la pamba bali ni watu
wenye kujali zaidi maslahi yao binafsi na
kwamba sehemu kubwa ya wanaolalamika
hawana mashamba.
"Tumefafanua sana jambo hili katika
vyombo vya habari juu ya utaratibu wa kulipa
shilingi milioni 50 kwa wanunuzi wa pamba
kwa kila kanda, na hii fedha inayotakiwa
kulipwa siyo sharti la mtu kupewa leseni bali
ni ya kulipia deni la pembejeo ambazo tayari
mfuko wa pembejeo umekopa."
"Wanaoendelea kulalamika siyo wakulima
halisi, maana wanadai sharti hilo litapunguza
wanunuzi, wao wanataka wanunuzi wawe
wengi, sasa uwingi wao wanataka wawe
wangapi? Wanasema tu bila kuelewa,"
anasema Bw. Bwahama.
Baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika
vya msingi wanasema imefika wakati serikali
hivi sasa iangalie uwezekano wa kuivunja
bodi iliyopo na iunde chombo kingine
mbadala kitakachoweza kumsaidia kikamilifu
mkulima wa zao la pamba.
Viongozi hao wanasema, imechangia kwa
kiasi kikubwa kuporomosha bei ya pamba
kwa mkulima kwa lengo la kuwasaidia
matajiri wanaonunua zao hilo ambapo
bodi hiyo imekuwa ikiruhusu mkulima
kurundikiwa mzigo mkubwa wa kodi.
Baadhi ya kodi zinazokatwa kutoka katika
kila kilo moja ya pamba anayouza mkulima
ni pamoja na asilimia tano sawa na shilingi 33
kwa kilo moja kama ushuru wa halmashauri
ya wilaya, ushuru wa kijiji asilimia moja,
gharama ya vituo vya ununuzi shilingi 45
kwa kila kilo moja ya pamba inayouzwa na
gharama za uchukuzi shilingi 45 kwa kilo.
Kodi nyingine ni gharama za uchambuaji
(ginning expenses) shilingi 100 kwa kila kilo
moja, benki shilingi 15 kwa kila kilo moja,
mfuko wa pembejeo shilingi 15 kwa kila kilo
moja anayouza mkulima na mfuko wa elimu
ambapo mkulima hukatwa asilimia tatu ya bei
iliyopo katika soko.
Kama hiyo haitoshi kilo moja ya pamba
inayouzwa na mkulima huyo pia hukatwa
asilimia mbili ya bei iliyoko katika soko
kama fedha ya tahadhari kwa tukio lolote
linaloweza kusababisha kuharibika kwa
pamba ikiwa haijasafirishwa.
Kwa mujibu wa maelezo ya viongozi wa
vyama vya ushirika vya msingi, wanunuzi
wa zao la pamba kabla ya kuanza kwa
msimu hukaa na kuangalia bei ya pamba
itakayokuwepo katika soko kwa msimu
husika na kisha huondoa gharama hizo na kile
kinachosalia ndiyo hupewa mkulima.
No comments:
Post a Comment