29 March 2012

Waziri Nchimbi kufunga michuano ya NSSF

Na Victor Mkumbo
WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt. Emmanuel Nchimbi anatarajia kuwa mgeni rasmi katika kilele cha mashindano ya NSSF Cup kwenye fainali zitakazofanyika Jumamosi, kwenye Uwanja wa TCC Sigara.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana Mratibu wa mashindano hayo, Juma Kintu, ilieleza kuwa kabla ya kufunga michuano hiyo hiyo Waziri Nchimbi, atapata fursa ya kuangalia fainali ya mechi ya soka kati ya Zanzibar na NSSF, wakati netiboli kutakuwa na mchezo kati ya Zanzibar na TBC.

Mratibu huyo alisema bingwa kwa upande wa soka atazawadiwa sh. milioni 3.5, wa pili sh. milioni. 2.5 na mshindi wa tatu ataondoka na sh. milioni 1.5.

Alisema kuwa washindi kwa upande wa netiboli wa kwanza atapewa sh. milioni 3, wa pili sh. milioni 2 na tatu ataondoka na sh. milioni 1, wakati wafungaji bora kwa michezo yote watapatiwa sh. 300,000.

Michuano ya mwaka huu, imeshirikisha timu 18 za mpira wa miguu na netiboli ambapo imechezwa kwa muda wa wiki tatu kwa mtindo wa makundi.

No comments:

Post a Comment