29 March 2012

Wabunifu watatu kuiwakilisha Tanzania South Afrika Fashion Week

Na Elizabeth Mayemba
WABUNIFU watatu, Doreen Estazia , Jamila  Swai na Evelyne Rugemalira wamepata nafasi ya  kwenda kwenye maonesho ya mitindo nchini Afrika Kusini,kupitia kampuni ya Millen Magese Group company Limited, maonesho hayo yanajulikana kama South Africa Fashion Week.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa kampuni hiyo Millen Magese alisema wabunifu  hao watapanda jukwaan Aprili Mosi katika onesho linalobeba jina la Tanzania International Fashion Exposé (TIFEX).

Millen alisema alipata fursa ya kutembelea wabunifu hao na kujionea jinsi walivyokuwa wabunifu katika fani hiyo na kuhamasika kuwachukua na kushiriki katika maonesho hayo maarufu ya mitindo katika bara la Afrika.

Alisema kuwa amevutiwa sana na jinsi walivyokuwa wabunifu na hivyo kuhamasika kuwapa nafasi hiyo ya kujitangaza kimataifa kwa mara ya kwanza, katika historia ya Tanzania kupitia mradi huo ambao pia dhumuni lake ni kutangaza vivutio vya utalii wa Tanzania kimataifa.

Alifafanua kuwa mpango huo pia una lengo la kuitangaza Tanzania kupitia fani ya mitindo dunia nzima, kama New York fashion week, London Fashion Week, Lagos Fashion week na Milan Fashion week.

Millen alisema kuwa hayo yanawezekana kutokana na uzoefu wake wa miaka nane katika fani ya mitindo na mahusiano mazuri kati yake wadau wa mitindo. Mbali ya wabunifu hao, Millen pia amewapa nafasi wanamitindo watatu, Anastazia Gura (21) na mapacha, Victoria Casmir (20) na Victor Casmir kuonyesha mitindo katika maonyesho hayo ya Afrika Kusini.

Wanamitindo hao wamepata nafasi hiyo baada ya kuwashinda wengine 486 waliofika katika usaili uliofanyika kwenye hoteli ya Serena chini ya majaji, Mustapha Hassanali, Ritha Poulsen na mwanamitindo maarufu Aminat Ayinde kutoka kampuni ya America  Next top model cycle 12.

Mbali ya wanamitindo hao Millen pia ameingia mkataba wa kufanya kazi na mwanamitindo wa kiume, Benard Chizi ambaye pia alishinda katika usaili huo na pia ataungana na wenzake kwenda Afrika Kusini.

Millen pia alionyesha kusikitishwa na wanamitindo maarufu ambao walikuwa wanawasiliana naye akiwa Afrika Kusini kutaka kusaidiwa kufika hatua za kimataifa. lakini cha kushangaza, wanamitindo hao, hawajajitokeza katika usaili huo na kumsononesha sana.

No comments:

Post a Comment