Na Rose Itono
WANAFUNZI wa Shule ya Msingi Bwawani ya Manispaa ya Ilala wameiomba Serikali iwapatie madawati ili waondokane na adha ya kukalia viroba.
Wakizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, walisema wamejikuta wakilazimika kukalia viroba kila siku kutokana na shule yao kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi.
Walisema kuwa idadi ya wanafunzi imesababisha madawati yaliyopo shuleni hapo kutokidhi mahitaji yao na kusababisha kero ya kuchafua nguo huku wengine wa kike wakitumia muda mwingi kujistiri ili wasikae uchi mbele ya walimu wao hasa wa kiume.
Mmoja wa wanafunzi wa darasa la tano katika shule hiyo ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema ili ukalie dawati lazima awe mbabe la vinginevyo kila siku atakaa chini.
"Ili ukalie dawatini lazima uwe mbabe bila ubabe utakaa chini miaka yote,"alisema.
Aliongeza kutokana na hali hiyo wanafunzi hulazimika kutoka majumbani kwao na viroba vya kukalia ili kuzuia nguo zao zisichafuke.
Awali Mkuu wa Shule hiyo Bi. Mayasa Khamis alipoitisha kikao cha wazazi kujadili mikakati ya kuongeza ufaulu alisema wanafunzi kukaa chini kunatokana na wengi wa wanafunzi.
Aliomba wazazi na wadau mbalimbali kushirikiana ili kuwezesha kununuliwa kwa madawati ya kutosha kwani kila darasa lina wanafunzi zaidi ya 70.
No comments:
Post a Comment