ELIMU ni uti wa mgongo katika ulimwengu wa sayansi na teknolojia ndiyo maana nchi mbalimbali duniani, zimewekeza katika elimu ili jamii kubwa isome na kuitumia elimu waliyonayo kwenye harakati za maendeleo ya Taifa, kuboresha ustawi wa jamii.
Taifa ambalo lipo nyuma kielimu, linakabiliwa na hali ngumu ya maendeleo katika nyanja mbalimbali. Upo umuhimu wa kuhakikisha elimu inayotolewa kwa wananchi, inakuwa bora na inakidhi mahitaji ya jamii husika.
Ni wajibu wa Serikali na wadau wa sekta hiyo, kushirikiana katika harakati za kuiwezesha jamii kubwa kupata elimu.
Ukweli ni kwamba, nchi mbalimbali zilizopiga hatua ya maendeleo, ziliona umuhimu wa kuwekeza katika elimu iliyojaa maarifa, uwezo mkubwa wa kufikiri, ubunifu, ujuzi, ufundi wa aina mbalimbali na kuvumbua dhana mpya.
Sisi tunasema kuwa, hiyo ndio nguvu ya elimu inayoleta maendeleo katika jamii. Wafadhili wametoa pesa nyingi kusaidia nchi maskini kama Tanzania lakini bado umaskini upo.
Jamii kubwa ya Watanzania inaishia katika lindi la matatizo ambayo nchi nyingi waliyatatua miongo kadhaa iliyopita. Wenzetu hivi sasa wanatafuta maarifa mapya ya kuibadili dunia wapendavyo kwa kurahisisha kila kitu kwa teknolojia na uvumbuzi mpya.
Imani yetu ni kwamba, suala la kuwekeza katika elimu bora haliepukiki bali linapaswa kutiliwa mkazo na kila mtu kwa kuzingatia umuhimu wake.
Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kusema elimu ndiyo msingi wa maendeleo ya Taifa lolote Duniani. Kuna aina mbalimbali za elimu ambazo mtu anazihitaji ili aweze kuendesha maisha yake ya kila siku.
Elimu ya ufundi stadi ndiyo inayopewa kipaumbele zaidi na wananchi wengi ili waweze kujiajiri au kuajiriwa. Elimu hiyo, huwawezesha wananchi kusoma masomo maalumu katika vyuo mbalimbali ufusti stadi na kupata maarifa mapya.
Ili nchi yetu ipige hatua ya maendeleo, ipo haja ya kila mwananchi kuona umuhimu wa kusoma na kuelimika.
No comments:
Post a Comment