27 March 2012

Walemavu waangukia wanawake viongozi

Na Anneth Kagenda
WANAWAKE viongozi wakiongozwa na Mama Salma Kikwete na Mama Anna Mkapa, wameombwa kusaidia makundi ya wanawake wenye ulemavu nchini ili waweze kufichua wenzao walioko mikoani ambao bado wamefichwa ndani.
Mwito huo ulitolewa Dar es Salaam jana na  Mwenyekiti wa Kikundi cha Wanawake Wajasiriamali wenye Walemavu Tanzania (FAMASA) Bi. Lilian Kabalika, kwenye semina ya siku moja iliyolenga kuwajengea uwezo wanawake na hatimaye kujitambua na kuondokana na utegemezi.

Alisema ni vyema viongozi hao wakajitokeza kuwafadhiri ili wawafikie wenzao mikoani kwani kuna wanawake walemavu ambao hawana mtaji wa kuuza maji ya sh. 50 au 100. Alisema hali hiyo inawafanya kunyanyapaliwa.

"Tofauti na walemavu walioko mikoani pia walemavu wanawake tumekuwa tukikumbana na changamoto nyingi ikiwamo ya walemavu kushindwa kupeleka watoto wao shule, hivyo kuishia kufanya kazi za ndani... tumeamua FAMASA iwasaidie watoto waende shule na ndio maana tunawaomba viongozi wanawake kutuwezesha," alisema Bi.Kabalika.

Alisema lengo lingine la kikundi hicho ni kutoka mahali walipo na kusonga mbele zaidi kutokana na walemavu wengi kubweteka huku wengi wao wakijiona hawawezi kufanya jambo lolote, hali inayowafanya washindwe kuthaminiwa.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni inayojihusisha na Mapinduzi ya Fikra Tanzania, Bw. Mark Msemwe, alisema mlemavu anayeweza kutoka sehemu moja kwenda nyingine ana uwezo wa kujishughulisha na kufanyakazi ya kumuingizia kipato.


No comments:

Post a Comment