27 March 2012

Kodi kwa wafanyabiashara ziboreshe miundombinu ya sokos



 Baadhi ya meza zilizohamwa na wafanyabiashara katika soko la Soko la Wakulima Kariakoo wakilamikia kutozwa ushuru mkubwa na Halamshauri ya Wilaya ya Nzega usiolingana na mapato ya shughuli zao. (Picha na Juma Kiyenze)
 Na Juma Kiyenze
MIGOGORO vurugu na migomo inayotokea katika jamii nchini hutokana na kuyumba kwa utawala bora unaokandamiza haki za wananchi, hali inayosababishwa na uroho wa kujilimbikizia mali.
Ingawa tunasema uongozi bora ni watu, ardhi, siasa safi na uongozi makini wenye kujali changamoto mbalimbali zinazoikumba jamii, bado watu wanaoteuliwa kuongoza hujiona wao ni miungu watu, kiasi cha kudharau wajibu wao kwa wananchi.

Matokeo yake jamii inapokosa uvumilivu kwa kutotekelezewa matatizo yanayowasibu, huamua kuchukua sheria mkononi kwa kuandamana na kuzusha vurugu, kuwakumbusha viongozi majukumu yao.

Maandamano hayo yanapozimwa na Jeshi la Polisi kwa usalama wa watu na mali zao, viongozi hao bado hawachukuliwi hatua za kinidhamu kwa kukiuka maadili ya kazi.

Nguvu ya umma inapofanya kazi zake, hakuna wa kuzuia, hata kama polisi watashika silaha, ingawa busara na hekima inapaswa kufuatwa kufikia muafaka wa kudumu.

Waswahili husema, 'ukiona moshi unafuka, ujue nyumba inaungua'. Hali ilivyo katika Soko la Wakulima Kariakoo lililopo eneo la Majengo wilayani Nzega, kutokana na wafanyabiashara wengi kuhama na wengine kugawanyika.

Kuhama kwao na mgawanyiko uliopo sokoni hapo unasababishwa na uongozi wake uliopo madarakani kwa zaidi ya miaka 20 sasa, bila ya kuchaguliwa wengine kuongoza, ili kupata fikra mpya zenye kujenga, kuleta umoja na kukabili changamoto mbalimbali zilizopo na zinazojitokeza kwa ushirikiano wa pamoja.

Kukuza uchumi usiosababisha uchafuzi wa mazingira hakutazuia ukuaji wa uchumi, bali kutaboresha mazingira ya viumbe, kutoa nafasi za ajira, kupunguza umaskini na kuhimiza usawa katika jamii.

Mwenyekiti wa Soko hilo, Bw.Ibrahim Musa, alikiri kuwepo kwa migogoro inayojitokeza ya kuhama kwa wafanyabiashara na kugawanyika kutokana na Halmashauri hiyo kutoza ushuru mkubwa wa shs. 4,000 kwa watu walio na meza na 6,000 kwa wauza ndizi, ambao unawaumiza kibiashara.

"Sisi wafanyabiashara wa ndani tunatozwa ushuru wa shs 4,000 na 6,000 kwa wauza ndizi ni mkubwa na hasara kwetu hauendani na mapato ya biashara zetu, ndio maana wengine wanahama kila siku na meza ni tupu kama unavyoziona", anasema.

Anasema, pamoja na kushindwa kulipa ushuru huo, ambao unawakandamiza, pia ni shinikizo la mmoja wa kiongozi  wa Halmashauri hiyo aliyetoa amri wahamie eneo lililokuwa likiuziwa pombe za kienyeji, maarufu 'Kachoma', ambalo halikidhi matakwa yao na ya walaji kiafya, halikuandaliwa na lina uchafu uliokithiri.

"Hiyo ilikuwa ni amri mtendaji mmoja kuwahamishia wakulima wa mbogamboga eneo la 'Kachoma', ambalo kiafya ni hatari na halifai kibiashara na pia wanakimbia ushuru wa soko ni mkubwa kwa manufaa ya viongozi hao", anafafanua.

Anaeleza kwamba, miundombinu na mazingira ya soko hilo ni machafu, hasa wakati wakati wa msimu wa mvua, maeneo mengi hutuwama matope na maji machafu, ambayo ni hatari kwa maisha ya wafanyabiashara na walaji.

Anasema halmashauri haijali mazingira hayo, isipokuwa kukusanya ushuru.

Uchunguzi uliofanywa uligundua hali ni mbaya na lilikutwa lundo la taka, ambalo halijazolewa na mamlaka husika kwa muda mrefu sasa kwa kisingizio cha ukosefu wa mafuta ya magari ya kuzoa taka zinazolishwa na wakazi wa mji.

Kwa upande wa eneo hilo, wafanyabiashara wengi wanalalamika kwa kunyanyaswa na viongozi wa Wilaya hiyo kwa kuwafukuza katika soko walilokuwa wakiuzia bidhaa zao, wala hataki kusikiliza changamoto zinazowasibu.

Pamoja na hayo, Mwenyekiti wa Soko la Wakulima, Bw. Musa maarufu ameiomba halmashauri hiyo kuboresha mazingira na miundombinu ya soko, ikiwamo kuchimba mifereji ya majitaka, uzoaji taka ngumu zinazozalishwa sokoni hapo ili kuepusha kutokea magonjwa ya milipuko.

Wafanyabiashara mbalimbali waliozungumza waliutaka uongozi wa soko hilo uitishe uchaguzi haraka, ili wachague viongozi wapya watakaokuwa mstari wa mbele kutatua kero zao.


Wamewataka viongozi walioshondwa kuendesha soko hilo kujiuzulu kwa kushindwa kuwatendea haki na kutatua kero mbalimbali zinazojitokeza ili kupisha uchaguzi mwingine watakaochagua viongozi bora watakaotetea masilahi yao na ya walaji.

Akieleza kero yake, Mfanyabiashara Bi. Stumai Mahamoud, anasema Halmashauri ya Wilaya ya Nzega wanafahamu kukusanya ushuru na siyo uwajibikaji, kwa visingizio mbalimbali.

Mfanyabiashara Bi. Sawisha Hassan mkazi wa Majengo, ambaye ni mwanzilishi wa soko hilo, walishiriki kujijengea maeneo ya kufanyia biashara kwa ahadi ya kurejeshewa gharama zao na halmashauri, ingawa uongozi haujafanya hivyo.

Wafanyabiashara wa soko hilo wanaomba uongozi wa halmashauri hiyo kuitisha mkutano sokoni hapo, ili wafahamu kero zao kwa amani na demokrasia na ushuru unaotozwa uangaliwe upya na uchangie kuboresha soko, vinginevyo watagoma kulipa.

Soko hilo halina vyoo kwa ajili ya wafanyabiashara kujisaidia haja kubwa na ndogo. Watu wengi walionekana kukojoa juu ya taka zinazozalishwa na kutupwa mita chache kutoka katika soko hilo.

Kimsingi uchafuzi wa mazingira haukubaliki katika dunia ya leo ya sayansi na teknolojia. Lakini serikali imezidisha mapambano dhidi ya janga hili linaloonekana la kimataifa.

Uharibifu huu wa mazingira upo wa aina nyingi, kuna ule unaotokana na kazi za jamii yetu inayotuzunguka pamoja na ule wa kutumia vifaa vyenye kemikali kali.




No comments:

Post a Comment