29 March 2012
Uharibifu mazingira kwa kukata miti waongeza umaskini
Uchomaji holela wa misitu unaweza kupunguza idadi ya wanyama ambao ni kivutio kwa watalii katika hifadhi za Taifa.
Na Semeni Masoud
UHIFADHI na usimamizi wa mazingira duniani na kitaifa una nia ya kushinda matatizo yanayotokana na umaskini, maradhi, hali mbaya na duni ya upatikanaji wa chakula, makazi machafu, maji yasiyo salama, upatikanaji wa nishati usioridhisha na ukosefu wa ajira.
Msukumo mkubwa wa uongozi wa mazingira ni kulinda sehemu asili ya kuishi binadamu na kuoanisha upungufu uliopo kwenye mazingira kusaidia kufikia maamuzi yanayohusu masuala na shughuli za uchumi.
Serikali ya Tanzania ilitambua hatari ya kupoteza rasilimali za nchi na hewa safi, mabaki ya mimea na wanyama wa kale, nyangumi, miti ya asili ambayo iko mbioni kutoweka.
Katika kurekebisha hali hiyo, serikali imechukua hatua thabiti kwa kutengeneza sera, sheria na mfumo wa taratibu ambazo zinaendana na masuala ya jamii, uchumi na siasa.
Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wameweka mkazo katika kuendeleza kukuza na kuhamasisha ushirikishwaji wa jumuiya na watu binafsi katika kuimarisha uhifadhi na uongozi wa mazingira.
Pamoja na hayo waliweka kampeni za kutambua umuhimu wa mazingira, elimu ya mazingira na kuendeleza ujuzi ambao ulisaidia katika kuhifadhi na kuendesha masuala ya mazingira.
Elimu ya mazingira nchini bado haijawafikiwa wananchi ndio maana wengi wao hususani wanaoishi jijini Dar es Salaam hawazingatii suala hilo.
Ni ukweli usiopingika kuwa, mazingira ni muhimu kwa kuwa, yanamzunguka mwanadamu. Kuna faida ya kutunza mazingira kwani inasaidia kuviendeleza viumbe hai katika jamii.
Kutotunza mazingira inapelekea, kupoteza viumbe muhimu na hali ya uchumi kuyumba kwani baadhi ya viumbe huwa ni kivutio kwa wageni kwenye mbuga za wanyama.
Mdau wa mazingira jijini Dar es Salam Bw. Brian Vitus anasema kuwa, kuna vyanzo vya uharibifu wa mazingira nchini.
Anaongeza kuwa, vyanzo hivyo ni ukataji wa miti ovyo, uchomaji wa misitu na kilimo cha aina moja kinazhosababisha mmomonyoko wa ardhi na kufanya mazao mengine yasiweze kuhimiri rutuba hiyo.
Bw. Vitus anasema kuwa, ukataji miti kiholela husababisha athari za kukosa mvua za kutosha kwa kuendesha shughuli za kilimo hali inayopelekea ukame na kimbunga kutokana na eneo kuwa wazi na kuleta athari katika jamii.
Anasema kuwa, ukataji wa misitu husababisha wanyama ambao ni kivutio nchini mwetu kutoweka.
Anasema, faida moja wapo inayopatikana katika misitu ni utalii ambao husaidia kuongeza pato la taifa na fedha za kigeni.
"Tukiangalia kwa namna moja au nyingine hifadhi za taifa (TANAPA), imekuwa na mchango mkubwa wa kudhibiti wanaochoma misitu ovyo na wanaovusha asili mali zetu hususani wanyama, " anasema Bw. Brian
Anasema, ili utalii uweze kukua na kuimarika ndani na nje wadau wa sekta hiyo, serikali na taasisi mbalimbali nchini zinatakiwa ziboreshe miundombinu ili wageni waweze kufika kwa urahisi kwenye vivutio.
Pia, usafiri wa kuwafikisha watalii kirahisi katika hifadhi kama ndege, barabara na majini unatakiwa kuboreshwa ili kuwavutia wengine.
Kukiwa na udongo wenye rutuba, mimea na wanyama wanaoishi katika hifadhi wataishi vizuri na sekta ya utalii itazidi kukua.
Uvuvi haramu umekuwa chanzo cha uharibifu wa vivutio vya majini na mazimgira ya bahari kuwa kuwa, kuna wanyama ambao ni kivutio kikubwa nchini wanaoishi ndani ya maji hivyo basi mazingira hayo yakitunzwa vizuri tutakuwa na hifadhi nzuri kwa kizazi cha kesho.
"Jua linasaidia kuzalisha mwanga na kuwapa vitamin d wanyama, pia husidia mimea kukua na kustawi vizuri hata hivyo pindi mvua itakaponyesha husaidia mimea kustawi na wanyama kujipatia maji kwa matumizi yao hivyo tutunze mazingira na wanyama waweze kupata makazi" anasema Bw.Vitus.
Viwanda vinachangia uharibifu wa mazingira kwa kiasi kikubwa kwa viumbe hai kwa kumwaga maji taka yenye kemikali pamoja na moshi unaokwenda angani na kuathiri viumbe hai.
"Ni ukweli usiopingika kwani sisi wenyewe tumekuwa mashahidi kutokana na wageni mbalimbali kuja kutembelea vivutio vyetu, kutokana na hali ya hewa kuwa nzuri, utulivu na amani uliopo hivyo tunatakiwa kuilinda ili kuongeza watalii na patola taifa," anasema Bw Brian.
Anasema kuwa, hifadhi za taifa zinatakiwa kuweka mkazo na kutunga sheria zitakazowadhibiti wanaoharibu hifadhi nchini ili kupunguza vitendo hivyo.
"Sheria iliyopo haitoshi kudhibiti uharibifu unaoendelea, naishauri mamlaka husika kuongeza adhabu ili kuendeleza vilivyoachwa na wazee wetu," anasema.
Tanzania ni moja ya nchi yenye vivutio vingi vya utalii ambavyo vikitumika vizuri tunaweza kuondokana na utegemezi uliopo hivyo tunatakiwa kishirikiana kuvitunza ili visaidie kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Sekta hiyo ni miongoni mwa sekta zenye uwezo wa kukuza kwa haraka uchumi. Inaongeza fedha za kigeni na kuajiri watu 30,000, na kuhamasisha sekta nyingine kama kilimo na viwanda.Mchango wake katika pato la taifa ni asilimia 14, ambayo ni sehemu ndogo ikilinganishwa na uwezo wa sekta hii.
Tanzania imebahatika kuwa na vivutio vingi vya utalii ilkilinganishwa na nchi nyingi kwa kuwa na wanyamapori wengi na wa aina nyingi na mandhari za kuvutia.
Vivutio vingi asilia na ukubwa wa nchi unatoa nafasi ya kuendeleza shughuli za utalii kama kutazama wanyama, safari na shughuli za ufukweni, upandaji milima, kuona mandari, uwindaji, na upigaji picha.
Sera ya utalii ya mwaka 1999 ina malengo ya kuongeza uchumi na kuleta hali nzuri kwa wananchi kwa kupunguza umaskini, kuendeleza utalii ulio endelevu na wa hali ya juu kiutamaduni, unaokubalika na watu, kwa kuzingatia mazingira mazuri.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment