Na Cornel Antony, Mtwara
MKUU wa Wilaya Nanyumbu mkoani Mtwara, Bi.Fatuma Ally amewaagiza wakazi wa wilaya hiyo kutafuta mwafaka wa maji safi na salama ili waweze kujihakikishia usalama wa kuyapata bila matatizo.
Hayo aliyasema hivi karibuni wakati akiweka jiwe la msingi kwenye tanki la maji katika Mradi wa Lukula wilayani Nanyumbu uliopo Kijiji cha Lukula Kata ya Masuguru ndani ya Tarafa Nanyumbu mkoa hapa.
Alisema, hali ya hupatikanaji wa maji safi na salama si nzuri kwani asilimia 27.1 ni ndogo sana na inakatisha tamaa.
Mkuu huyo alisema, umefika wakati wa kuvuna maji ya mvua kwani wilaya hiyo ina nyumba nyingi za mabati zenye uwezo wa kuvuna maji ya kutosha katika kaya.
"Siyo hivyo tu, pia tuanzishe mifuko ya maji kila kijiji na kuimarisha mifumo ya maji iliyopo ili iwe yenye uwezo ya kutoa huduma ya maji kikamilifu," alisema Mkuu huyo.
Bi.Fatuma aliongeza kuwa wanaweza kuanzisha mifuko hiyo ya maji kupitia kwenye mazao ya choroko, karanga ufuta na korosho.
"Kama wenzetu wa Tandahimba na Newala huchangia sh.10 kwa kilo moja katika miradi mbalimbali ya maendeleo na sisi umefika wakati wa kuiga mazuri ya wenzetu, tujitoe na Serikali yetu iko tayari kusaidia kujenga miradi mingine mikubwa ya maji," alisema.
Awali Mhandisi wa Maji wilayani humo, Bw.Emanuel Chuma alisema, Wilaya ya Nanyumbu inategemea vyanzo vya maji yalipo chini ya ardhi hususan visima virefu.
"Ambapo wilaya ina visima 162 vya kati, visima 26 vifupi na visima 16 virefu.
Visima vinne vina mtandao wa maji na visima 18 vinatarajiwa na mtandao wa maji, tuna mradi wa Lukula wenye mtandao wa vijiji 10 Sengenya, Mara, Ulanga, Chipuputa, Chivirikiti, Holola, Najembo, Ndechela, Ndwika na Lukula," alisema Bw. Chuma.
Mbali na hayo uchunguzi wa Majira umebaini kuwa kila mwananchi anao wajibu wa kutunza vyanzo vya maji vinavyomzunguka kuanzia kaya hadi taifa ili kujihakikishia usalama wa maji.
Pia utunzaji wa vyanzo vya maji hususan kupanda miti katika maeneo ambayo yanachemchem au yanazungukwa na visima ili maji hayo yaweze kuwa safi na salama.
Katika hatua nyingine huduma ya maji safi na salama inasaidia wananchi kujiepusha na milipuko ya magonjwa hasa kipindupindu na kuhara.
No comments:
Post a Comment