23 March 2012

Tuondoe kasoro zilizopo kwenye sekta ya kilimo

NENO ‘Kilimo Kwanza’ ni kauli mbiu ambayo inawahamasisha wakulima nchini kuongeza juhudi kwenye kilimo cha kisasa ili kuinua kiwango cha uzalishaji mazao ya chakula na biashara.
Serikali ya Awamu ya Nne, chini ya Rais Jakaya Kikwete ipo katika utekelezaji wa mpango huo wenye lengo la kuleta mapinduzi ya kijani katika sekta hiyo kiuchumi na kijamii.

Tangu kuanza kwa mpango huo, zipo kasoro nyingi zilizojitokeza ambazo zinastahili kutatuliwa mapema ili tusipoteza maana halisi na kushindwa kuleta mapinduzi yanayokusudiwa kwa mkulima.

Baadhi ya wadau wa kilimo, wamekuwa wakionesha wasiwasi wao wa kufanikiwa kwa mpango huo na kuleta mapinduzi ambayo yanayokusudiwa kutokana na kasoro zilizopo.

Wadau wa kilimo wamekuwa wakisisitiza kuwa, bila kutatua kasoro zilizopo mpango huo hauwezi kufanikiwa kama inavyotarajiwa.

Sisi tunasema kuwa, Tanzania bado ina safari ndefu ili kufanikisha mpango huo. Dhamira na utashi katika mpango huo ni nzuri ili kuleta mapinduzi ya kilimo lakini vikwazo bado ni vingi.

Mpango huu upo kisiasa zaidi na tatizo kubwa linaloweza kuufanya ukakwama ni ukosefu wa miundombinu kwa wakulima nchini. Miundombinu hiyo ni pamoja na ile ya barabara hasa ziendazo vijijini kwenye mazao ambazo hazipitiki kirahisi.

Hali hiyo inachangia pembejeo zishindwe kufika sokoni kwa wakati pamoja na baadhi ya viongozi serikalini na wataalamu wa kilimo, kushindwa kuwafikia wakulima vijijini na kuwapa elimu ya kilimo cha kisasa jambo linalochangia malengo ya mpango huo kukwama.

Kukosekana kwa soko la uhakika la mazao ya wakulima, huchangia mazao mengi kuharibika kabla ya kufika sokoni ili mkulima apate faida badala yake huingia hasara.

Jambo jingine linaloweza kukwamisha mpango huo ni baadhi ya wakulima kutofahamu mbinu za kisasa za uvunaji na uhifadhi wa mazao yao kabla ya kufikishwa sokono.

Imani yetu ni kwamba, ili mkulima apate mazao yenye kukubalika kwenye soko, wataalam wa kilimo wanapaswa kuwa karibu na wakulima badala ya kukaa ofisini kama wanavyofanya sasa.

Wataalamu hao wanatakiwa kuwa karibu na wakulipa kwa kuwapa mbinu za kilimo bora cha mazao ya chakula na biashara na Serikali kuweka mpango maalumu wa kuboresha barabara.

No comments:

Post a Comment