23 March 2012

Nyumba 53 kubomolewa Kariakoo leo

Na Heri Shaban
SERIKALI Mkoa wa Dar es Salaam leo alfajiri inatarajia kuanza kubomoa nyumba 53 zenye familia 106 zilizokuwa za Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Shirika la Reli Tanzania ( TRC), zilizopo eneo la Kariakoo, ili kupisha ujenzi wa miundombinu ya mabasi yaendayo kasi.
Uamuzi huo ulitangazwa Dar es Salaam jana na Mkuu wa Mkoa huo, Bw. Saidi Mecky Sadiki, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Alisema kuwa agizo la kuvunja nyumba hizo inatokana na Mahakama Kuu kutupilia mbali maombi ya wakazi hao waliofungua kesi wakipinga kuondolewa kwenye nyumba hizo, ambazo awali waliuziwa TPA na TRL.

"Kazi ya kubomoa nyumba hizo itafanywa na kampuni ya udalali ya Yono Auction Mart kuanzia alfajiri chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi kwa ajili ya kudumisha usalama, lakini halitahusika na uvunjaji," alisema Bw. Sadiki.

Wakati wa operesheni hiyo barabara ya Lindi na Msimbazi zote zitafungwa kwa muda ikiwa ni sehemu ya kudhibiti usalama wakati ubomoaji utakapokuwa ukiendelea.

Aliwataka wakazi wa nyumba hizo waondoke na kuacha nyumba hizo zikiwa wazi, kwa kuwa jana mahakama ilitupilia ombi lao la kutaka nyumba hizo zisibomolewe.

Kwa mujibu wa Bw. Sadiki tangazo la utwaaji ardhi ambayo imepangwa kujengwa kituo cha mabasi DARTS lilitolewa na waziri mwenye dhamana Aprili 4, 2008 likieleza madhumuni husika na muda wa mtu yeyote anayedai kuwa na haki na ardhi hiyo kuweka pingamizi.

Aliongeza kuwa baada ya muda uliotajwa kwenye tangazo kumalizika, Kamishna wa Ardhi alimwandikia Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala kuwa hakuna mtu au taasisi yeyote iliyowasilisha madai au maelezo katika ardhi husika.

Aliongeza kuwa baada ya hapo Rais alifuta hati za wamiliki wa viwanja hivyo na kuongeza kuwa taratibu za utwaaji ardhi hiyo zimekamilika kama sheria inavyojieleza.

Alisema amri ya utwaaji maeneo yaliyo katika namba 2446/208 na 2445/208 kitalu A Mtaa Msimbazi na Lindi, ilitolewa katika tangazo la Serikali namba 193 LD/153946 na 151870 ni batili na kinyume cha sheria.

4 comments:

  1. hiyo barabara haijaisha hadi leo?
    Who is behind this slow move of the nation?

    ReplyDelete
  2. Tungependa sana serikali yetu nayo ikawa miongoni mwa nchi zinazojitahidi kwa miundo mbinu hasa suala la usafiri kwa ujumla. Ni matumaini yetu kuwa kukamilishwa kwa mikakati hiyo hatutakuwa na magari yaendayo kasi tu lakini pia tutakuwa na barabara zinazoruhusu magari hayo kupita yaani suluhisho la foleni kwa ujumla. HONGERENI VIONGOZI WETU!

    ReplyDelete
  3. Ni mikakati mizuri lakini lolote laweza kutokea maana viongozi wa Tanzania wana vichwa vya wendawazimu. Pale kipawa watu walibomolewa kwa ajili ya kupanua uwanja wa ndege mpaka leo ni hadithi eti yule mfadhili kajitoa... hala hala na hii ya magari kasi tukapewa story kama hiyo..

    ReplyDelete
    Replies
    1. Ina maana hata serikali inaweza kuwa na mipango kama ya >kombolela> mchezo ule wa watoto? Iweje mfadhili aingie mkataba nao kisha ajitoe? Ni lini tutafika? Mungu ibariki Africa, Mungu ibariki Tanzania!

      Delete