23 March 2012

'Tutaendelea kusaidia kukuza uchumi'

Na Willbroad Matias
SERIKALI ya Tanzania imeahidiwa kuendelea kupewa ushirikiano katika miradi yote ya maendeleo kwa lengo la kuisaidia kukuza uchumi wa nchi.
Ahadi hiyo ilitolewa na meneja uhusiano na masoko wa Benki Exim (T), Bi. Linda Chiza, wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa jengo la biashara la ghorofa 20 la Muungano wa Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo Tanzania (TFC)  jijini Dar es Salaam juzi.

Mradi huo umefadhiliwa kwa kiwango cha sh. bilioni 12 na benki hiyo  na wafadhili wengine .

Bw. Chiza alisema kuwa mapema mwaka huu benki yake ilisaini makubaliano na shirikisho hilo ambayo mbali na masuala mengine, yatachangia kufanyiwa matengezo kwa jengo la Ushirika la zamani lenye ghorofa 12 lililopo karibu na jengo jipya linaloendelea kujengwa.

“Tunajivunia kuwa sehemu ya chachu ya maendeleo nchini, mkopo wetu kwa TFC hautasaidia kuleta maendelo katika Jiji la Dar es Salaam pekee, bali nchi nzima kwa ujumla,"alisema Bi. Linda na kuongeza;

“Tutaendelea kusaidia miradi mbalimbali endelevu pamoja na kuchangia maendeleo ya jamii inayotuzunguka katika maeneo tunayofanyia kazi kupitia mpango wetu maalum wa kuisadia jami."

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TFC, Bw. Hassan Wakasuvi wakati wa tukio hilo alisema kuwa shirika lake limeshakusanya sh. bilioni 25 kwa ajili ya mradi mzima ambao unatarajia kukamilika katika kipindi cha miaka miwili.

Alitaja wawekezaji wengine kwenye mradi huo kuwa ni Dhamana ya Uwekezaji Tanzania (UTT). Hata hivyo aliongeza kuwa mkopo huo utarejeshwa ndani ya kipindi cha miaka mitano chini ya usimamizi wa UTT kabla ya TFC kuwa mmiliki kamili.

Bw. Wakasuvi pia alitoa shukrani zake kwa taasisi za fedha zilizochangia katika mradi huo huku akiwa na matumaini makubwa kuwa mradi huo utakuwa chachu ya maendeleo ya TFC kupitia mapato yatakayokusanywa pamoja na ajira mbali mbali.

Alifafanua kuwa; "Mradi huu utasaidia kutuzalishia mapato ili kusukuma mbele maendeleo ya shirikisho baada ya kumalizika. Tunawapongeza  wenzetu wa mashirika ya fedha kwa kutuamini na tunatarajia kuwa katika nafasi nzuri ya kurejesha mkopo huu kupitia mapato," alisema.

 

No comments:

Post a Comment