29 March 2012

Singida wahofia dampo kuhifadhi fisi, harufu

Na Damiano Mkumbo, Singida
WAKAZI wa Kijiji cha Munung’una Halmashauri ya Wilaya ya Singida wamelalamikia kero ya uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na umwagaji wa takataka kutoka mjini Singida ambao walidai unaweza kusabisha madhara kiafya sambamba na kuhifadhi wanyama wakali hasa fisi.
Wananchi wa kijiji hicho kilichopo mpakani mwa halmashauri hizo mbili, walidai kuwa sasa umwagaji wa takataka hizo uliyokuwa unafanyika eneo la Kijiji cha Manga Manispaa ya Singida sasa unazidi kusogea katika makazi yao hasa Mnung’una.

“Tunakerwa na harufu mbaya, moshi, inzi wengi kuingia katika nyumba zetu, kuchafua vyanzo vya maji na kufanya maisha yetu yawe katika hatari ya kukumbwa na milipuko ya magonjwa," alidai mmoja wa wakazi hao.

Walisema, kutokana na hali hiyo pamekuwa na fisi wengi kwenye sehemu hiyo yenye vichaka hivyo kuhatarisha maisha ya binadamu na mifugo hasa mbuzi na kondoo, pamoja na wanafunzi wanaotoka upande wa kusini kuelekea shuleni kulazimika kusindikizwa na wazazi wao.

Waliomba dampo hilo liondolewe ili kuepusha madhara zaidi yanayoweza kuwapta wananchi hao ya kuharibu afya zao na kupoteza mifugo yao kwa kuliwa na fisi.

“Takataka zinazidi kutupwa na kulundikwa huko na huko kiasi cha kusogea kwenye makazi na kufunga njia muhimu inayokatiza kutoka sehemu moja na kwenda sehemu zingine za kijiji chetu,” alieleza Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mnung’una kijijini hapo Bw.Juma Mtinda.

Walisema, wamepeleka malalamiko yao kuhusu kero hiyo katika ngazi mbali mbali kuanzia kata ya Msisi hadi wilayani, lakini bado hawajaona hatua yoyote iliyochukuliwa kwa kumaliza tatizo hilo.

Akizungumza kuhusu suala la umwagaji wa takataka katika eneo la Kijiji cha Manga, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida Bw.Yona Maki alisema eneo hilo limetengwa kisheria lenye hekari 10.8 na sasa limeanza kuzungushiwa ukuta wa matofali ya seruji.

“Hakuna takataka zinazotupwa nje ya eneo hilo lililopo mpakani, kando ya barabara ya Singida kwenda Mwanza lililoanzishwa tangu mwaka 2004 umbali wa kilomita 16 toka mjini Singida ambalo halikuwa na watu," alisema.

Alisema, atafanya uchunguzi ili kubaini iwapo kuna hali yoyote inayoonesha kusogezwa kwa eneo la dampo hilo na kuingia katika Kijiji cha Mnung’una ili kuweza kufikia utatuzi wake.

No comments:

Post a Comment