29 March 2012

'Mpango wa DASIP kurejesha ndoto'

Na Faida Muyomba, Mwanza
SERIKALI kupitia Mpango wa Maendeleo ya Kilimo Wilayani (DASIP) imesema inatarajia kutumia sh. bilioni 550 kujenga masoko saba ya Kimataifa katika wilaya zilizopo mipakani.

Mratibu wa DASIP Kanda ya Ziwa, Bw. Charles Tulahi aliyasema hayo jana katika mkoani Mwanza wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema, ujenzi huo utahusisha wilaya za Kasulu Kijiji cha Mananila, Tarime Kijiji cha Remagwe na Kahama Kijiji cha Busokwa.

Wilaya nyingine ni pamoja na Karagwe katika Kijiji cha Nkwenda na Moro, Misenyi katika eneo la Mtukula pamoja na Ngara eneo la Kabanga.

Alisema, ujenzi huo unatokana na wakulima wengi kuwa na mazao ya kutosha ya chakula na biashara baada ya kupata mafunzo ya kilimo bora lakini wanakosa mahali pa kuuzia mazao hayo.

Alisema, ujenzi huo wa masoko utawanufaisha walikuma wengi ambao walikuwa wakikumbwa na matatizo ya udanganyifu uliokuwa ukifanywa na madalali na kujikuta wakiuza mazao yao kwa bei ya hasara na kumnufaisha mlanguzi.

“Masoko hayo yatakuwa na maeneo makubwa kadri biashara itakavyo kuwa inapanuka, halmashuri husika zitachukua majukumu ya kupanua masoko hayo badala ya kuyahamisha katika sehemu nyingine hivyo lengo la Serikali kuanzisha mpango huu ni kuwatafutia masoko ya uhakika wakulima wake,”alisema.

Alisema, katika masoko hayo kutakuwa na huduma mbalimbali ikiwemo zile za kibenki na sehemu ya kubadilishia pesa na kumfanya mkulima kuweza kutunza fedha zake katika mahali salama baada ya kuuza mazao yake.

Pia alisema, wakulima hao watapata fursa ya kufahamu taarifa za masoko na bei ya mazao katika masoko mengine yakiwemo ya ndani na hata ya nje ya nchi hivyo kuimarisha biashara zao.

Alisema, ujenzi huo unatarajia kuanza mapema Oktoba mwaka huu na kukamilika mwishoni mwa mwaka 2013.

No comments:

Post a Comment