16 March 2012

Nyerere: Mkapa aombe radhi wananchi

*SAU kushinikiza Tendwa ajiuzulu kwa kushindwa kazi
Queen Lema na Pamela Mollel, Arumeru

MAMENEJA Kampeni wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), katika uchaguzi mdogo Jimbo la Arumeru Mashariki, mkoani Arusha, Bw. Vincent Nyerere, amemtaka Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu Bw. Benjamin Mkapa, awaombe radhi wananchi wa jimbo hilo kwa kuwadanyanya juu ya uhusiano wake na familia ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Bw. Nyerere alisema katika msiba wa Mwalimu Nyerere, Bw. Mkapa alimpa rambirambi kama mwanafamilia sasa anaposema hana uhusiano na Mwalimu Nyerere ni kuudanganya umma na wakazi wa jimbo hilo.


“Kutokana na matamshi ya Bw. Mkapa ni wazi kuwa ameudanganya umma na wakazi wa jimbi hili hivyo anapaswa kuomba radhi kwani jamii kubwa itamshangaa kama atashindwa kufanya hivyo kama kiongozi mstaafu.

“Ni vyema akaja jimboni Arumeru na kueleza ukweli kuhusu uhusiano wangu na familia ya Mwalimu Nyerere ili kusahihisha usemi wake,” alisema Bw. Nyerere.

Kwa upande wake, Mbunge wa Karatu kwa tiketi ya CHADEMA, Mchungaji Israel Natse, alisema kama Bw. Mkapa atashindwa kuomba radhi kwa wakati, watapita maeneo yote ya jimbo hilo kukanusha uongo huo.

Alisema chama hicho kipo tayari kupokea msamaha wake kama atakiri kufanya makosa ya kuudanyanya umma.

Wakati huo huo, kampeni za uchaguzi mdogo katika jimbo hilo zimezidi kuchukua sura mpya baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuwataka wananchi kutoichagua CHADEMA kwa madai makada wa chama hicho walishangilia msimba wa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Marehemu Jeremiah Sumari.

Mratibu Mkuu wa kampeni za CCM jimboni hapa, Bw. Mwigulu Nchemba, aliyasema hayo jana wakati akihutubia wananchi wa Kata ya Makiba, eneo la Valeska.

Alisema miongoni mwa makada walioshagilia kifo hicho ni pamoja na mbunge wa Arusha Mjini, Bw. Godbless Lema na kusisitiza kuwa, CHADEMA haina huruma na wakazi wa jimbo hilo hivyo mgombea wao Bw. Joshua Nassari hapaswi kupewa uongozi.

“Naomba niwaulize, mtu mwenye huruma anaweza kuja msibani na kushangilia wakati mna machungu ya kuondokewa na mbunge wenu, msiwape kula kwani hawana ubinadamu,” alisema.

Mwisho.


8 comments:

  1. Hapo tuwe wakweli wenye uchungu huwa ni wananchi au ndugu wa marehemu!isitoshe hakuna anayeshangilia kifo cha mtu hata walikuwa na ugomvi hao CCM waache kuwazuga wananchi kwani wao hawakuwepo msibani?waeleze sera zao za kuwanyang'nya wananchi rasilimali zao.

    ReplyDelete
  2. Kwani hao CCM wamekosa mambo mengine ya kuwaambia wananchi hadi ifike mahali wanakuja na sera change kiasi hiki? Tunaona ajali mbaya, vifo masipitalini watu tunalia haka kama alopata ajali humjui, haitamwingia akilini hata motto wa chekechea kuwa kuna MTANZANIA anaeweza kucheka msiba UNLESS akili yake si sawasawa. ACHENI POROJO CCM, MWAGENI SERA,

    ReplyDelete
  3. Mimi ninachowashangaa wale watanzania wanaoshhabikia ccm,nashindwa kabisa kueleza hivi hawaoni au hawasikii au hawana akili.Hivi kweli hawa ccm wametufikisha hapa tulipo katika hali mbaya,halafu leo hii tena uwasupport ndo ujue nchi yetu watu tuliomo hatuna maono kabisa.Uongozi wa ccm umechoka kila kila kitu.Wataeleza nini jipya kwa watu wa Arumeru?wameuza migodi ,mikataba feki,ununuzi wa rada,ufisadi,epa, haya yote ni matatizo tena makubwa na hawa wote waliofanya haya yote wanatamba mitaani na magari mazuri,pesa nyingi,kodi zetu.Na bado sisi tunashangilia eti ccm.Hivi tuna akili au kamasi.???????Wale wote waliosaini mikataba mibovu watapeta tu.Na hakuna atakaye chukuliwa hatua kwa uongozi wa ccm.Mpaka chadema ichukuwe dola,hapo ninauhakika watu waliohusika kuwajibishwa.WaTANZANIA SIO MBUMBUMBU.Itafika mwisho,siku ipo yaja.Ahsante.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Sioni dalili ya CCM kuachia hii Dola kwa kuangalia namna ya upinzani unaoendelea. Fujo nyingi! Kutaka madaraka kwingi!hasira N.K. Dola ina hatari ya kudumu kwenye CCM miaka 40 ijayo.

      Delete
  4. Wana Arumeru fungukeni, msibumbazwe na vikofia/khanga/wali/mashati/sh 5'000. Hivyo ni vitu sana sana vya mwezi au miwili tu, lakini litawagharimu maisha yenu kwa miaka mitano. wa kusikia na asikie

    ReplyDelete
  5. Inapofikia Mkuu wa nchi mstaafu anakosa sera na kuzungumzia watu/mtu, hapo ni tatizo kubwa. Na mhasibu wa chama tawala anaposema matukio ya mitaani kuwa ni kama sera, napata mashaka. Hivi CCM hawana mtu mwenye kuzungumzia 'IDEAs, VISION' nk?

    ReplyDelete
  6. Nimesoma habari hii sikuelewa kabisa kilichoandikwa ni mara yangu ya kwanza kusoma sasa ninapoambia Mkapa aonmbe radhi sijui amefanyaje, habari haikuwa na background ya habri ya kwanza, kama mwandishi kakosea hata mhariri naye pia, Majira mmekwisha kabisa hamna wahariri hapo, mnacheza tu.

    ReplyDelete
  7. this is politics ! let them propel ! kuomba radhi maana yake nini !

    ReplyDelete