Bw. Salum Mtondoo
Na Mwajuma Juma, Zanzibar
MWAKILISHI wa Jimbo la Bububu kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Magharibi Unguja, Zanzibar Bw. Salum Amour Mtondoo (49), amefariki dunia.
Bw. Mtondoo ambaye alikuwa Mwakilishi wa Jimbo hilo baada ya kuibuka mshindi katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2010, alifariki jana katika Hospitali ya Riufaa Mnazi Mmoja kwa maradhi ya moyo.
Taarifa iliyotolewa na Baraza la Wawakilishi, ilisema marehemu alisumbuliwa na maradhi hayo kwa muda mfupi ambapo Spika wa baraza hilo Bw. Pandu Ameir Kificho, aliwapa pole wakazi wa jimbo hilo kwa kuondokewa na mwakilishi wao.
“Tunamuomba Mwenyezi Mungu aijalie familia ya marehemu pamoja na wananchi wa Jimbo la Bububu katika kipindi hiki cha msiba,” alisema Bw. Kificho.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Bw. Vuai Ali Vuai, alisema msiba huo sio wa chama hicho pekee au wakazi wa Jimbo la Bububu bali ni wa Taifa zima.
“Tumepokea msiba huu kwa masikitiko makubwa lakini tuelewe kwamba, hii ni kazi ya Mungu haina makosa, jambo la msingi tuwe na subira,” alisema Bw. Vuai.
Marehemu alizaliwa tarehe Desemba 14,1962 huko Bububu, Wilaya ya Magharibi na kupata elimu ya msingi na Sekondari katika Shule ya Bububu kuanzia mwaka 1969-1979.
Enzi ya uhai wake, marehemu aliwahi kufanyakazi ya usimamizi wa Kiwanda cha COTEX mwaka 1983-1985 na baadae kufanya kazi za ujenzi katika ushirika wa BBB mwaka 1986-1992.
Mwaka 1992-2010 alikuwa akifanya kazi zake za biashara ambapo kisiasa, marehemu amewahi kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya CCM ikiwemo Ujumbe wa Kamati ya Siasa ya Tawi na Ujumbe wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya na Mkoa.
Marehemu ameacha wake wawili (vizuka) na watoto 10. Mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi Amin.

No comments:
Post a Comment