21 March 2012

Njaa yasababisha wananchi kugombania matunda porini

Na Phesthow Sanga, Singida
 WANANCHI wa Kata
ya Kidaru wilayani
Iramba Mkoa wa
Singida wameiomba
Serikali kuwapatia chakula cha
msaada kutokana na kukabiliwa na
njaa kali hali inayosababisha kuishi
kwa kula matunda mbalimbali ya
porini.

Ombi hilo la wananchi lilitolewa
juzi na Diwani wa kata hiyo,
Bw.Kiselei Mpinga wakati akitoa
taarifa ya hali ya njaa kwa Mkuu wa
Wilaya ya Iramba, Bi.Grace Mesaki
ofisini kwake.
Diwani Mpinga alisema,
kutokana na kukosekana kwa mvua
msimu wa kilimo wa mwaka 2011,
2012 wananchi wanakabiliwa na
njaa katika maeneo ya vijiji vitatu
vya Kidaru, Tyegelo na Luono.
Alisema, hivi sasa wananchi
wanakula matunda aina ya mikulu
na midokedoke ambayo ni jamii ya
matunda aina ya matongo.
Alisema, watoto wamekuwa
wakila ilimradi ni matunda hali
inayoweza kuwafanya kula matunda
mengine ambayo si kwa matumizi
ya binadamu na hivyo kupata athari
mbalimbali ndani ya miili yao.
Kwa upande wake Mkuu wa
Wilaya ya Iramba, Bi.Mesaki
alikiri kuwepo kwa tatizo la njaa
katika Kata ya Kidaru lakini
akasema kuwa serikali ilipeleka
chakula cha msaada katika maeneo
hayo kwa awamu mbili kwa watu
waliofanyiwa sensa.
Hawa viongozi wa Kata ya Kidaru
ni waoga kwani licha ya serikali
kupeleka chakula hicho, viongozi
wao waligawa kwa kila mwananchi
hata wale ambao hawakuwa na
tatizo la njaa, kwa hiyo utaona ni
woga wa hawa watu, kwa hiyo
idadi ya waliotakiwa kupewa
chakula ikaongezeka na hivyo
kusababisha chakula kutotosha,"
alisema Mkuu huyo.
Hata hivyo Mkuu huyo ambaye
hivi sasa anakaimu pia nafasi ya
Mkuu wa wilaya za Manyoni na
Singida, alikiri kuwa Serikali bado
haijaleta chakula katika awamu ya
tatu kama walivyoahidiwa na wako
katika kukisubiri chakula hicho ili
wananchi waweze kugawiwa kwa
kuzingatia wale waliofanyiwa
sensa tu na si vinginevyo.
Alisema, kutokana na uzembe
huo wa viongozi wa Kata ya Kidaru
kugawa ovyo chakula hicho kwani
kama wangefuata maelekezo
ya serikali ya kila mwananchi
aliyefanyiwa sensa kupewa kilo
200 bado wananchi wangekuwa na
akiba ya chakula hadi pale kingine
kitakapoletwa tena.
Kutokana na tatizo hilo la njaa
Kidaru, Mkuu huyo wa Wilaya
amewaagiza maofisa tarafa saba za
wilaya hiyo kufanya tathimini ya
hali ya njaa katika maeneo yao na
kumletea taarifa mapema ili naye
aweze kuifikisha mkoani kwa ajili
ya utekelezaji.
Hivi karibuni Mbunge wa Jimbo
la Iramba Magharibi, Bw. Mwigulu
Nchemba alitembelea kata hiyo
ambapo wananchi walimuomba
afikishe kilio chao cha njaa kwa
serikali.

No comments:

Post a Comment