21 March 2012

Mtama mweupe wazidi kupata soko

Na Jovither Kaijage,Ukerewe
 WAKULIMA wilayani
Ukerewe, mkoani
Mwanza wamehimizwa
kulima zao la mtama kwa wingi
kwa kuwa kuwa limepata soko
kubwa

Hayo yalisemwa na Ofisa
Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika
wa Halmashauri ya Wilaya ya
Ukerewe, Bw. Samson Ibraimu,
katika kikao cha kamati ya ushauri
ya wilaya hiyo chini ya Mwenyekiti
Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Bi.
Queen Mlozi.
Alisema hivi sasa mtama
mweupe unatakiwa kwa kiwango
kikubwa na kwenye viwanda viwili
vya kutengeneza pombe vya jijini
Mwanza , ambapo kwa mwaka
vinahitaji kati ya tani 900 hadi
1,200 za mtama mweupe.
Alisema viwanda hivyo pia
katika kipindi hicho cha mwaka
vinahitaji tani 100 hadi 150 za
mtama mwekundu.
Akifafanua zaidi alisema mbali
ya zao hilo kuhimili hali mbaya ya
hewa, pia litawawezesha wakulima
kupata chakula cha kutosha na
kuwaingizia kipato kutokana na
kuwepo soko la uhakika.
Akielezea zaidi alivitaja viwanda
hivyo kuwa ni kiwanda cha bia cha
Serengeti na kile cha Uniplastic
Tanzania kinachotengeneza pombe
ya Tingisha.
Kutokana na hali hiyo alisema
Mkoa wa Mwanza umetenga tani
60 za mbegu ya mtama mweupe
ziuzwe kwa ruzuku ya Serikali,
ambapo mkulima ananunua kilo
moja kwa sh. 800 baada ya Serikali
kuweka ruzuku ya sh. 700.
Aliwataka wakulima wa kanda ya
ziwa kutumia fursa hiyo kulima zao
hilo kwa wingi kwa maelezo kuwa
linaweza kuwa mbadala la biashara
na chakula.

No comments:

Post a Comment