29 March 2012

Mazao yaozea shambani- Makete

Na Rashid Mkwinda, Makete
IDADI kubwa ya matunda yaliyoiva wilayani Makete mkoani Njombe yanaozea shambani kutokana na ubovu wa barabara na hivyo kuchangia  wakulima kukosa kipato na kushindwa kuchangia maendeleo.
Matunda yanayolimwa wilayani humo ni pamoja na Zabibu,Peasi,Furusadi na tufaa ambayo yanaozea mitini na mengine kugeuzwa kuwa chakula cha nguruwe na ndege.

Mwandishi wa habari hizi alipata fursa ya kutembelea vijiji vya Ipelele, Mbanga, Kidope na Makaranga vilivyopo katika tarafa ya Magoma na kushuhudia idadi kubwa ya matunda yakiwa yanaozea mitini na kuliwa na ndege.

Wakizungumzia athari hizo baadhi ya wanakijiji waliozungumza na gazeti hili walisema kuwa serikali imeisahau wilaya hiyo na kushindwa kuisaidia kujenga barabara mbovu za kuingia na kutoka wilayani humo.

Mkulima mkazi wa Kijiji cha Kidope kilichopo katika Kata ya Iniho Bw.Anyosisye Fungo alisema  matunda yamezagaa mitini kutokana na wafanyabiashara wenye uwezo wa kununua kushindwa kufika katika kijiji hicho sababu ya barabara mbovu hivyo wanaiomba serikali kuboresha miundo mbinu ili kuwasaidia wakulima.

‘’Tunaishi katika mazingira magumu hatuna kipato kingine zaidi ya kutegemea kilimo, tunaomba tusaidiwe ili tujikwamue na kumudu kuchangia maendeleo’’alisema Bw.Fungo.

Akizungumzia matatizo yanayowakumba wakulima Ofisa Mtedandaji wa Kata Ipelele Bi. Anna Sanga alisema kuwa wakulima wanajitahidi katika kilimo na zao pekee wanalotegemea kuboresha kipato chao ni pareto.

Alisema kuwa yapo mazao mengine ya biashara kama vile matunda na viazi mviringo hata hivyo yanashindwa kusafirishwa kutokana na wafanyabiashara kushindwa kuingia vijijini humo wakati wa masika kutokana na ubovu wa barabara.

Naye Ofisa Kilimo wa Kata ya Ipelele Bw.Samson Mwambungu alisema kuwa asilimia kubwa ya eneo la vijiji vya wilaya hiyo viko milimani ambako ndiko wakulima wa mazao ya chakula na biashara na kwamba tatizo
lililopo ni barabara za kuunganisha vijiji hivyo.

Naye Mbunge wa Jimbo la Makete Dkt. Binilith Mahenge akizungumza kwa njia ya simu kutokea Jijini Dar es salaam alisema kuwa tatizo la miundo mbinu wilayani Makete lipo katika mpango wa miaka mitano ijayo na kwamba kupitia mkoa mpya wa Njombe barabara za Njombe-Makete na Makete –Kitulo hadi Mbeya zitatengenezwa kwa kiwango cha lami .



No comments:

Post a Comment