29 March 2012

Migogoro ya ardhi inaweza kupoteza amani tuliyonayo

MIGOGORO ya ardhi nchini imekithiri na kusababisha umwagaji damu. Ni wazi kuwa migogoro hiyo imegawanyika kwenye makundi mawili moja likihusisha wakulima na wafugaji, jingine linahusisha wananchi na wawekezaji.
Kimsingi migogoro inayohusisha wananchi na wawekezaji inachangia wananchi kuichukia serikali yao.

Katika maeneo mengi yaliyohusishwa na migogoro ya ardhi, tayari kumetokea vurugu zilizosababisha uvunjifu wa amani hata kusababisha vifo.

Vurugu hizo pia zimetokea kwenye maeneo ambayo udugu na kuvumiliana vilitawala lakini hadi sasa, hakuna jitihada za haraka zilizofanywa na Serikali kumaliza migogoro hiyo.

Hatua zinazochukuliwa ni zile za kujaribu kutuliza hasira za wahusika jambo linaloweza kutuletea maafa makubwa baadaye.

Sisi tunasema migogoro mingi ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji inatokana na makundi hayo kutotengewa maeneo.

Mtu akipata eneo mahali popote anajenga, kulima au kufuga kwa sababu Serikali haijachukua hatua stahiki ya kutenga maeneo na matumizi yake.

Ili kuepuka mapigano ya mara kwa mara na kutunza mazingira, umefika wakati wa Serikali kutenga maeneo ya kilimo, ufugaji, makazi ya watu na yale ya wazi.

Maofisa ardhi ni miongoni mwa watu wanaochangia migogoro hiyo kwa kuuza maeneo zaidi ya maara moja hivyo kusababisha jamii kugombaana hata kuchukiana.

Sababu kubwa inayochangia maofisa hao kusababisha migogoro ya ardhi ni tamaa ya fedha huku wakijua wanachokifanya ni kinyume na maadili ya kazi zao.

Imani yetu ni kwamba, ardhi ni mali ya mwananchi na Serikali hivyo kila upande unapaswa kushirikishwa wakati wa kuuza au kumtafuta mwekezaji.

Umefika wakati wa maofisa hao kubadilika na kufanya kazi kwa mujibu wa sheria ili kupunguza migogoro ya ardhi ambayo inachangia wananchi kuichukia Serikali yao.

No comments:

Post a Comment