- Mradi hewa wa machinjio watumia bilioni 2.7/=
KAMATI ya Hesabu za Serikali za
Mitaa (LAAC), imebaini ufisadi
mkubwa wa fedha uliofanywa
kwenye mradi wa ujenzi wa
machinjio ya ng’ombe ambao ulibainika kuwa
hewa hivyo kuisababishia Serikali hasara ya
sh. bilioni 2.7.
Ufisadi huo ulibainika Dar es Salaam jana
wakati kamati hiyo ikifanya kikao cha mapitio
ya hesabu za Halmashauri ya Kinondoni.
Kutokana na hali hiyo, watu wote waliohusika
na mradi huo watalazimika kwenda kujieleza
kwa Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda wakati
wa kikao cha bunge mjini Dodoma ambacho
kinaratajiwa kuanza Aprili mwaka huu kabla ya
kuchukuliwa hatua.
Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti
wa LAAC, Bw. Augustino Mrema, alisema
lazima watu hao wachukuliwe hatua za kisheria
ili iwe fundisho kwa wengine.
Awali Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo,
Bw. Idd Azzan, alisema kuna sh. milioni 223
ambazo zilitolewa na manispaa hiyo ili kuchangia
ujenzi wa machinjio ya kisasa kwenye eneo la
Gongolamboto lakini hadi sasa haijulikani
zimetumikaje.
Alisema uongozi wa Jiji ulitoa kiwanja ili
kujengwa machinjio ya kisasa na ndio walikuwa
wasimamizi wakubwa lakini hadi sasa hakuna
dalili za ujenzi.
"Kuna mradi ambao ulishirikisha Manispaa
zote za Dar es Salaam kwa kuchangia fedha
ambapo Halmashauri ya Temeke, ilitoa sh.
milioni 224, Ilala sh. milioni 364 na Jiji zaidi
ya sh. bilioni moja ambapo jumla ya fedha zote
zilikuwa sh. bilioni 2.7," alisema.
Akitoa majumuisho ya kamati hiyo, Bw. Mrema
alisema kamwe suala hilo haliwezi kuvumiliwa
kwani Serikali inafilisiwa kwa kuingia mikataba
hewa wakati mradi hauonekani.
Aliongeza kuwa, haiwezekani watu wachache
wafanye ubadhirifu wa mamilioni ya fedha za
wananchi na kuendelea kudunda mtaani.
"Hawa watu tutawaita Dodoma mbele ya
Waziri Mkuu watuambie huu mradi upo wapi,
kamwe hatuwezi kunyamazia suala hili na kukaa
kimya," alisema Bw. Mrema.
Akizungumza na waandishi wa habari juu ya
tuhuma hizo, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dkt.
Didas Masaburi, alisema madai kuwa fedha hizo
ziliishia kwenye uongozi si ya kweli.
Alisema kampuni iliyopewe jukumu la kujenga
machinjio ya East Afrika Meat Company, iliishia
kufanya upembuzi yakinifu na tayari imefilisika
hivyo kushindwa kujua nani wa kumdai.
No comments:
Post a Comment