27 March 2012

Mgombea APPT-Maendeleo aahidi neema Kigamboni

Na Mwandishi Wetu
MGOMBEA nafasi ya udiwani kata ya Vijibweni Kigamboni jijini Dar es Salaam, kwa tiketi ya APPT Maendeleo, Bw. Abdalah Nasoro, ameahidi kuwaleta neema wakazi wa kata hiyo iwapo watamchagua katika uchaguzi mdogo wa siku ya Jumapili.
Aliyasema hayo wakati akizungumza na gazeti hili kuhusu mikakati yake ya kuwatumikia wananchi wa kata hiyo ambao wana tatizo kubwa la barabara.

Uchaguzi mdogo katika kata hiyo unafanyika kufuatia kifo cha aliyekuwa diwani wake, Bw. Noran Dewji, wa Chama cha Wananchi (CUF) mwaka jana.

Bw. Nasoro alisema yeye ni mkazi wa vijibweni hivyo anafahamu vyema matatizo ya wakazi wa kata hiyo. Aliwaomba wananchi wamwamini na wampe kura za kishindo siku ya Jumapili.

“Kata ya vijibweni kuna viwanda tisa, lakini wananchi hawanufaiki na uwepo wa viwanda hivyo, nawaahidi wakinichagua nitasimamia mapato yatokanayo na viwanda yatumike kuleta maendeleo,” alisema

Alisema wajawazito na watoto ambao kwa mujibu wa maelekezo ya serikali wanapaswa kupata huduma bure wamekuwa wakilazimishwa kwenda na vifaa hospitalini jambo ambalo halitakiwi.

“Nitasimama kidete kuhakikisha wanawake wajawazito na watoto chini ya miaka mitano wanapata huduma bure kama wanavyostahili, haiwezekani ruzuku inatolewa na fedha haijulikani zinakwenda wapi”alisema.

Kuhusu mradi wa Kigamboni City, Nasoro alisema atajitahidi kama diwani wa kata hiyo kuhakisha anakuwa na taarifa kuhusu kinachoendelea na kuwajulisha wananchi.

“Miaka inakatika na wananchi kule hawaelezwi kinachoendelea, watu wanashindwa kuendeleza maeneo yao lakini hakuna taarifa zozote wanazopewa, mfano mtu ana chumba kimoja familia imeongezeka na anataka kuongeza kingine haruhusiwi,” alisema.

No comments:

Post a Comment