27 March 2012
Waliohama CUF wapata usajili
Kaimu Mwenyekiti wa Muda wa Chama cha Alliance For Democratic Change (ADC) 'Dira ya Mabadiliko' Bw. Said Miraji akibebwa na wanachama na mashabiki wa chama hicho mara baada ya kupata cheti cha usajili wa muda, Dar es Salaam jana.(Picha na Prona Mumwi)
Na Rehema Maigala
CHAMA kipya kilichoanzishwa na baadhi ya viongozi pamoja na wananchama waliojiengua kutoka Chama cha Wananchi (CUF) cha Alliance For Democratic Change (ADC), jana kimepata usajili wa muda.
Awali viongozi wa chama hicho kilipeleka maombi ya kuanzisha chama kipta kwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Bw. John Tendwa, Februari 7 mwaka huu.
Akikabidhi hati ya usajili wa muda, Bw. Tendwa alisema amefanya hivyo baada ya chama hicho kufuata taratibu zote zinazotakiwa.
Alisema chama chochote cha siasa lazima kiwe na wawakilishi kutoka Tanzania Bara na Zanzibar na kufanya mikutano ya kutafuta wanachama wanaotakiwa hivyo kimepewa siku 180 kwa ajili ya kutimiza masharti hayo.
“Kama chama hiki kitakosa wawakilishi, tunaweza kukifuta wakati wowote ule na kitakiuka sera zilizopangwa,” alisema Bw. Tendwa na kuongeza kuwa, baada ya kupata usajili wa muda chama hicho kitaruhusiwa kufanya mikutano na kina pamoja na haki ya kupata ulinzi kutoka Jeshi la Polisi.
Aliongeza kuwa, hawataruhusiwa kushiriki katika uchaguzi wa aina yeyote kwani bado hawajapata usajili wa kudumu.
Akizungumzia suala la bendela wanayotumia, Bw.Tendwa alisema ina rangi nyekundu, bluu, nyeupe na nyeusi ikifanana kidogo na ile ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
“Kama kutakuwa na minong'ono ya aina yeyote, itabidi wakae pamoja ili ibadilishwe,” alisema Bw. Tendwa.
Baada ya kupokokea usajili wa muda Kaimu Mwenyekiti wa Muda Bw. Abdallah Juma Kilaghai, aliwashukuru Watanzania kwa kuwaunga mkono hadi walipofikia.
"Chama changu kimepata usajili wa muda hivyo nitatimiza sera zote zinazotakiwa na pia nitaendesha mikutano kwa heshima zote bila ya kusema chama kingine na bila ya kutoa matusi katika mikutano ya hadhara,"alisema Kilaghai
Alisema katiba yake haijaacha nyuma wanawake na walemavu kwa ajili ya kuwatetea mambo mbalimbali yanayowakabili nchi.
Tukio ya kupokea hatia ya usajili wa muda ilitawaliwa na shamrashamra ambapo maandamamo yalianzia Buguruni hadi ofisi za Msajili wa Vyama vya Siasa. Maandamano hayo yaliongozwa na pikipiki na magari.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment