21 March 2012

Kilimo bora kitaongeza uzalishaji malighafi viwandani


              Pamba ikiwa tayari kuvunwa
Na David John
KILIMO ni moja ya shughuli muhimu zinazofanywa na binadamu ili kupata mahitaji ya kila siku na kumudu gharama za maisha.
Historia, mila na thamani za watu katika jamii zinatokana na ustawi wa maendeleo ya sekta hiyo.

Sekta hiyo ni msingi wa maendeleo ya nchi mbalimbali duniani katika kukuza uchumi na kuinua kipato cha wananchi.

Nchi zilizowekeza katika sekta hiyo zimefanikiwa kuondokana na tatizo la uhaba wa chakula kwa wananchi wake.

Umuhimu wa sekta hiyo, umesababisha wataalamu na wadau mbalimbali wa kilimo kutafuta njia ya kuboresha mazingira ya sekta hiyo ili kuwafanya wakulima waongeze uzalishaji bila kuharibu ardhi.

Dhana iliyopo juu ya kilimo kinachofaa bila kuharibu rutuba ni moja ya sababu inayowafanya wataalamu katika sekta hiyo kuwa na tofauti kubwa miongoni mwao.

Wafanyabiashara wamekuwa wakihamasisha wakulima kutumia mbolea ya chumvi chumvi na dawa ya kuulia wadudu katika mazao kupitia matangazo mbalimbali ili kuongeza uzalishaji wa mazao.

Kwa upande wao, wataalamu katika sekta hiyo wamekuwa wakihamasisha wakulima kutumia mbole zenye kemikali ambapo wataalamu wa kilimo hai wanapinga mpango huo kwa madai kuwa,  kilimo hicho kina haribu ardhi nzuri yenye rutuba.

Kanuni zinazotumika katika kilimo, zinahusisha mtazamo wa watu juu ya udongo, maji, mimea na wanyama katika kuzalisha, kuandaa na kusambaza chakula na bidhaa nyingine.

Siasa za Tanzania zinachangia kukwamisha wakulima kufahamu umuhimu wa kilimo hai na kukiendeleza. Kampuni za nje, ndizo zinazonufaika kwa kutangaza matumizi ya mbolea zenye kemikali na dawa za kuulia wadudu ambazo zinachangia kuharibu ardhi.

Zinachangia kutangaza kampuni kubwa zinazosambaza dawa za kilimo na mbolea ndio sababu ya kuwepo kwa matangazo mengi yanayoshawishi wakulima kutumia bidhaa hizo.

Wakulima wa Tanzania hawapewi nafasi ya kuchagua njia zinazofaa kwa kilimo wanachokifanya kama ilivyo katika nchi nyingine.

“Tunataka kuwepo na uwiano katika kuhamasisha njia gani wakulima wanapaswa kuitumia katika kilimo na ufafanuzi wa njia hizo,”

Viongozi waliopo madarakani, wanafahamu faida na umuhimu wa kilimo hai lakini wanahofia kuhamasisha wakulima kwa sababu za kisiasa. Hali hiyo inachangia kilimo hai kionekane kimepitwa na wakati jambo ambalo halina ukweli wowote.

Nchi nyingine ambazo zinazojihusisha na kilimo cha kisasa, wakulima wao wanafahamu aina ya udongo wanaotumia na kiwango cha mbolea ya chumvu na dawa kwa kufuata utaratibu na kuwafanya wafanikiwe.

Wakulima wa Tanzania ni vigumu kupata mbolea inayoweza kuwatosheleza hivyo wengi wao wanatumia mbolea chini ya kiwango na kusababisha uharibifu.

Wapo baadhi ya wakulima wanaoelewa madhara yatokanayo na matumizi ya dawa hizo lakini wengi wao hawafahamu madhara yake hivyo wakipatiwa elimu wataona umuhimu wa kutumia mbolea ya asili.

Kilimo hai kina kanuni nne ikiwemo ya mazingira asilia ambayo huchangia hukiwezesha kilimo kuwa endelevu, huweka msingi wa kilimo hai kwa kuhusisha na uhifadhi wa mazingira kwani uzalishaji wa mazao unapaswa kuzingatia na kujali uhai wa udongo.

Ufugaji wanyama kwa kuzingatia mfumo wa mazingira ya shamba, ufugaji wa kuhama hama na utaratibu wa mavuno ya mazao pori, unapaswa kuendana na mzunguko wa kiikolojia na uwiano asilia wa mazingira.

Kilimo hai kinapaswa kufanikisha uwiano wa mazingira kwa kubuni na kuhimiza mfumo wa uzalishaji unaoweka mazingira bora kwa makazi na kutunza urithi wa kimaumbile na kilimo.

Kanuni ya afya inataka kilimo hai kuwa endelevu na kudumisha rutuba ya udongo, kuboreshe afya ya mimea, wanyama na binadamu.

Afya ni mfumo wa uhai na taratibu za maisha kama magonjwa, kutunza mwili,  akili, ustawi wa jamii, mazingira bora na mazuri ya kuishi, uwezo wa kujikinga na kushiriki katika uumbaji ni tabia za msingi na muhimu kwa afya bora.

Kanuni za kilimo hai zinazuia matumizi holela ya mbolea, dawa za wadudu au magonjwa ya mifugo na viatilifu au vinasaba vinavyoongezwa katika hifadhi ya vyakula ambavyo vinaweza kusababisha madhara ya kiafya kwa mlaji au mtumiaji.

Kanuni nyingine ni haki kwa watu wote ambao wanajihusisha na kilimo hai lazima wazingatie uhusiano wenye usawa katika ngazi zote bila upendeleo iwe kwa wazalishaji, walaji, wasindikaji, wafanyakazi, wafanyabiashara na wasambazaji ili kuboresha mazingira na kuhifadhi maliasili na rasilimali.

Anaongeza kuwa, mfumo wa kilimo hai unapaswa kubadilika na kuendana na matakwa ya hali ya ndani au nje ya mazingira husika.

Wanaojihusisha na kilimo hai wanapaswa kuongeza ufanisi na tija katika uzalishaji pasipo kuleta athari za kiafya na ustawi kwa kufanya tathmini na uchambuzi wa teknolojia mpya na zilizopo.

Uamuzi wa teknolojia na pembejeo gani zitumike katika kilimo lazima uzingatie amali na mahitaji ya wote wanaoweza kuathirika, hivyo ni muhimu kuwahusisha katika mchakato ulio wazi na shirikishi wakati wa kuchambua na kuchagua teknolojia.

Katika baadhi ya maeneo kama Singida, Tabora na Iringa wakulima wengi hutafuta mbolea hasa ya chumvi chumvi na kuzitumia katika ardhi inayoonekana kuzeeka lakini matatizo mengi huibuka kutokana na matumizi ya pamoja na dawa za kemikali kwenye kilimo.

Mbolea hizo na dawa za kuua wadudu zina madhara yake kwani zina sumu isiyoonekana inayoliwa au kunywewa na ndizo zinazoleta madhara kwa binadamu na udongo.

Mbolea asili ya mboji inaweza kupatikana au kutengenezwa kutokana na mazao yanayolimwa kwenye mazingira tunayoishi, mbolea hizo ni rahisi kurudisha udongo katika hali ya rutuba na asili yake.

Serikali haitoi umuhimu kilimo hai japo ndicho kilimo kilichotunza ardhi yetu na kuongeza uzalishaji wa malighafi.



























No comments:

Post a Comment