22 March 2012

Kikwete kufungua Kongamano la Utafiti wa REPOA

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Rais Jakaya Kikwete anatarajia kufungua Kongamano la 17 la utafiti wa Taasisi ya Utafiti ya Kupunguza Umaskini Nchini (REPOA), Jumatano wiki ijayo jijini Dar es Salaam.
Mkutano huu utatilia mkazo aina ya mageuzi ya kijamii na kiuchumi yanayopaswa kufuatwa na Tanzania ili kuongeza kasi ya kupunguza umasikini nchini..

Kwa mujibu wa taarifa toka REPOA, ukuaji wa uchumi wa Tanzania katika muongo mmoja uliopita umefanikiwa kupunguza umaskini kwa kiwango kidogo sana.

“Hata hivyo, uzoefu wa karibuni umeonyesha kwamba nchi nyingine zinazoendelea zimeweza kufikia mapinduzi ya uchumi na kupunguza umaskini kwa kiwango kikubwa,” anasema Mkurugenzi Mtendaji, Prof. Samuel Wangwe katika taarifa kwa vyombo vya habari jana jijini Dar es Salaam.

Alisema mkutano huo ulioandaliwa na REPOA utaangalia mafunzo yanayopatikana kutokana na uzoefu huo toka nchi mbalimbali wa jinsi ya kuwa na mapinduzi ya kijamii na kiuchumi ili kupunguza umaskini kwa haraka zaidi pamoja na kuangalia nafasi ya dola, sekta binafsi na jamii kwa ujumla katika kufikia lengo hilo.

Prof. Wangwe alisema katika taarifa yake kwamba kama ilivyo katika mikutano kama hiyo iliyopita, mada kuu mwaka huu itawasilishwa na kujadikiwa na magwiji katika eneo hilo.

Mtoa mada mkuu katika mkutano huo wa mwaka huu anatarajiwa kuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Tanzania, Dkt. Phillip Mpango.

Kati ya wageni maarufu katika taaluma ya elimu na utafiti mwaka huu ni Prof. Do Duc Dinh ambaye ni  mkuu wa idara ya mafunzo ya nchi zinazoendelea, katika taasisi inayohusika na uchumi wa dunia toka nchini Vietnam Nam na Prof. Li Xiaoyun ambaye ni  mtafiti mwandamizi katika Kituo cha Kimataifa cha Kupunguza Umaskini toka jijini Beijing, China.

Wataalamu hawa wataendesha mijadala itakayolenga kuonyesha jinsi baadhi ya nchi zilivyoweza kufanikiwa kupunguza umaskini kwa kiwango kikubwa baada ya kuwepo kwa mabadiliko makubwa ya kijamii na kiuchumi.

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof. Benno Ndulu anatarajiwa kuwa mwenyekiti katika kuongoza mjadala huo.

Mada mbalimbali zitakazotolewa zinatarajiwa kugusa maeneo sita muhimu kwa mabadiliko ya maendeleo.  Maeneo hayo ni pamoja na kuongeza tija katika kilimo, mageuzi ya utoaji wa huduma katika sekta ya umma, na viwanda.

Maeneo mengine yatakuwa ni uendeshaji wa raslimali, ajira na mitaji ya uwekezaji toka nje.

No comments:

Post a Comment