22 March 2012

Business Times kwa raha zao Robo fainali

Na Victor Mkumbo
TIMU za Kampuni ya Business Times LTD, 'The Bize FC' na 'The Bize' juzi zimetinga hatua ya robo fainali ya michuano ya NSSF Cup, baada ya kushinda mechi zao katika mechi zilizochezwa katika viwanja TCC Chang'ombe na DUCE, Dar es Salaam.
The Bize FC iliyonga hatua hiyo baada ya kuichapa Tumaini kwa mabao 4-3 katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa DUCE, Chang'ombe.

Nayo The Bize Queen ilifanikiwa kutinga hatua hiyo, baada ya kuinyuka Global Publishers mabao 37-7 katika mechi iliyofanyika viwanja TCC.

Katika mchezo wa soka na uliokuwa na upinzani mkubwa, Tumaini walianza kwa kulishambulia lango la wapinzani wao ambapo dakika ya pili walipata bao la kwanza kupitia kwa Henri Mlaya kutokana na uzembe wa mabeki wa The Bize.

Baada ya bao hilo, The Bize walijipanga na kufanya mashambulizi makali ambapo dakika ya tatu walisawazisha bao kupitia kwa George Denis, baada ya kuachia shuti la mbali lililojaa wavuni moja kwa moja.

The Bize iliandika bao la pili dakika ya 14, ambalo lililowekwa kimiani na Jemedar Said kwa njia ya penalti, baada ya kuchezewa faulo kwenye eneo la hatari.

Dakika ya 34 Tumaini walisawazisha bao la pili kupitia kwa Mlaya, baada ya kupiga shuti la mbali.

Wakitandaza kandanda soka safi, The Bize walipata bao la tatu dakika ya 38 kupitia kwa Sunday George, baada ya kuwatoka mabeki na kuukwamisha mpira wavuni ambapo matokeo hayo yalidumu mpaka mapumziko.

Kipindi cha pili Jemedari wa The Bize, alicharuka na kuwa mwiba mkali kwa Tumaini baada ya kupachika bao la nne dakika ya 57 kwa mkwaju wa penalti, baada ya kukwatuliwa na beki katika eneo la hatari.

Tumaini walipata bao la tatu dakika ya 88 kupitia kwa Denis Isike, baada ya mabeki wa The Bize kujichanganya na kukwamisha mpira wavuni.

The Bize, wanatarajia kushuka uwanjani kesho kumenyana na Habari Zanzibar katika mchezo wa robo fainali utakaopigwa kwenye Uwanja wa TCC.

Nayo The Bize Queens iliweza kutumia vyema wafungaji wake, Saliketa Mhina pamoja na Rehema Mohamed kukwamisha mabao katika mechi hiyo.

The Bize Queens baada ya ushindi huo, nayo itashuka dimbani kesho kumenyana na Uhuru Queens.


No comments:

Post a Comment