22 March 2012

TSPCA ya piganga uchinjiaji wa kikatili nchini

Na Stella Aron
WACHINJAJI katika machinjio mbalimbali nchini wameshauriwa kuacha tabia ya uchinjaji wa wanyama huku wanyama wengine wakishudia.
Hayo yamesemwa jana Dar es Salaam na katibu mtendaji wa Chama Cha Kuzuia Ukatili kwa wanyama Tanzania (TSPCA),Bi.JOhari Gesani alipokuwa akizungumza na Majira.


Alisema kuwa uchinjaji wa wanyama huku wanyama wengine wakiona ni sawa na kufanya ukatili kwa wanyama na ni kosa kisheria.

"Ng'ombe haruhusiwi kuona ng'ombe mwenzake akichinjwa lakini hivi sasa ukienda kwenye machinjio utaona ng'ombe anachinjwa huku wengine wakishuhudia hivyo ni sawa na ukatili kwa wanyama, " alisema katibu huyo.

Alisema ili kukomesha tabia hiyo tayari wameanza uhamasishaji dhidi ya ukatili kwa wanyama kwa nchi nzima.

Bi. Gesani alisema mkoa wa Dar es Salaam umekuwa ni mkoa wa kwanza katika uhamasishaji ambapo wamekuwa wakiwashirikisha watu mbalimbali wakiwemo wanasheria, wafugaji, wenyeviti wa serikali za mitaa na wachinjaji.

Alisema mpango huo wa kuhamasisha jamii kufahamu sheria dhidi ya ukatili kwa wanyama ni wa miaka mitatu ambapo wana imani kuwa baada ya kukamilika kwa mpango huo unaweza kupunguza kero hiyo.

"Kwa kipindi cha miaka mitatu cha uhamasishaji tuna imani kuwa ukatili dhidi ya wanyama nchini utapungua, " alisema katibu mtendaji huyo.

Hata hivyo alisema hivi sasa ukatili dhidi ya wanyama umekuwa kero ambapo wamekuwa wakitumika na kuuawa kwa imani mbalimbali.

No comments:

Post a Comment