22 March 2012

Alichofanya DC Tarime, hakistahili kama kiongozi

MWAKA 2009, Rais Jakaya Kikwete alimvua madaraka na kumfukuza kazi aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, mkoani Kagera, Bw. Albert Mnali, kutokana na kitendo cha kuwacharaza bakora walimu wa shule za msingi wilayani humo.
Bw. Mnali aliamrisha polisi kuwacharaza walimu viboko akiamini kuwa wao ndio walichangia wanafunzi wa darasa la saba wilayani humo kufanya vibaya katika mitihani yao ya mwisho.

Hatua hiyo, ilipingwa vikali na wanaharakati wakidai walimu hao walidharirishwa kijinsia na kuwavunja moyo kiutendaji.

Tukiachana na hilo, wiki iliyopita Mkuu wa Wilaya ya Tarime, mkoani Mara, Bw. John Henjewele, anadaiwa kumpiga na kumjeruhi mdogo wake wa kuzaliwa tumbo moja ambaye amefahamika kwa jina la Bi. Rose Henjewele.

Inadaiwa kuwa, chanzo cha tukio hilo ni Bw. Henjewele kutaka kuwapora nyumba waliyonunua kwa fedha za urithi wa nyumba ya marehemu baba yao iliyopo Mbezi, Dar es Salaam.

Kutokana na kipigo hicho, Bi. Rose alifungua kesi ya shambulizi katika Kituo cha Polisi Kawe na kupewa RB namba KW/RB/2442/2012.

Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Charles Kenyela, alisema hadi sasa jeshi hilo linamshikilia Bi. Gloria Henjewele ambaye inadaiwa alishiriki kumpiga Bi. Rose na kumjeruhi.

Ukweli ni kwamba, tukio hili limemdharirisha Bw. Henjewele kutokana na nafasi yake kama kiongozi anayestahili kuwa mfano katika jamii hata kama suala hilo lina sura ya kifamilia.

Sisi tunasema kuwa, Bw. Henjewele amepoteza sifa ya kuwa kiongozi wa mfano, ipo haja ya Rais Kikwete kumchukulia hatua hasa kwa kuzingatia kuwa, kutokana na nafasi haye hakupaswa kufanya mambo ya aibu tena kwa mdogo wake.

Kama leo hii kiongozi huyo ameweza kumpiga na kumdharirisha mdogo wake wa kuzaliwa tumbo moja, upo uwezekano mkubwa wa kufanya tukio kama hilo kwa watumishi anaowaongoza hali inayoweza kusababisha wananchi kuichukia Serikali yao.

Ili jamii iendelee kuwaamini wasaidizi wa rais na kuipenda Serikali yao, upo umuhimu mkubwa wa Bw. Henjewele kuchukuliwa hatua stahiki na mwajili wake ili iwe fundisho kwa wengine.

Imani yetu ni kwamba, Rais Kikwete atalipa uzito suala hili ili kulinda heshma ya Serikali na chama anachokiongoza kwa kuhakikisha kuwa, hatua atakayochukua jamii wataipokea bila manung'uniko yoyote kama ilivyo sasa.

Jeshi la Polisi    Mkoa wa Kinondoni, lihakikishe Bw. Henjewele anakamatwa na kufunguliwa mashtaka kama wanavyofanya kwa watuhumiwa wengine ambao makosa yao hayalingani na hili lakini jeshi hilo linatumia nguvu kubwa kuhakikisha waanakamatwa.

3 comments:

  1. huyo kiongozi ni vema achukuliwa hatua za kisheria na pia jamani askari muwe mnatumia akili ya ziada wewe mtu hawezi kukwambia ufanye kitu ambacho ni kinyume na sheria na ukizingatia askari ndio law enforcers so I don't understand what they are doing.

    ReplyDelete
  2. Hivi mnadhani tunaserikali????????

    ReplyDelete
  3. vyeo vya kupeana kwa kukutana barabarani ndo shida yake. haviangalii maadili ya mtu ila ushikaji

    ReplyDelete