09 February 2012

Yanga rahaa...utamu

*Yaichapa Mtibwa 3-1, yaongoza ligi
Na Elizabert Mayemba

HABARI ndio hiyo!ndivyo utakavyoweza kusema baada ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga kukwea kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo baada ya kuifunga Mtibwa Sugar mabao 3-0 katika mechi iliyopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Yanga inaongoza ligi hiyo kwakuwa na idadi kubwa ya mabao ya kufunga ambapo ina mabao 28 na Simba ina mabao 25 licha ya kuwiana kwa pointi zote zina pointi 34.

Pamoja na kuwiana kwa pointi lakini pia zinawiana kwa tofauti ya mabao zote zikiwa zina mabao matano na kuifanya Simba ishuke mpaka nafasi ya pili na Azam FC ipo katika nafasi ya tatu kwa pointi 31.

Yanga ilianza kuonesha uchu wa mabao mapema dakika ya saba kutokana na mshambuliaji wao, Davies Mwape akiwa pekee yake langoni alipiga mpira na kugonga mwamba na mabeki kuondosha hatari.

Mtibwa ilijibu shambulizi hilo dakika 30 kupitia kwa Said Rashid aliyepiga mpira wa adhabu lakini kipa Shaaban Kado alipangua.

Mtibwa ilipata pigo kwa kuwa pungufu baada ya mwamuzi Ibrahimu Kidiwa wa Tanga kumuonesha kadi nyekundu Saidi Mkopi kwa kumkwatua Stephano Mwasika.


Timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu na mpaka dakika 45 za kwanza zikimalizika timu hizo hazikufungana.

Kipindi cha pili kilianza kwa Mtibwa kuliandama lango la Yanga na dakika 46, Hussein Javu alikosa bao la wazi baada ya kupiga shuti lililogonga mwamba na kuokolewa na mabeki.

Mtibwa iliongeza kasi ya mashambulizi na dakika ya 60, Vincent Barnabas alifunga bao lakini mwamuzi msaidizi alilikataa kwa madai alikuwa tayari ameotea.

Baada ya mashambulizi hayo, Yanga ilitulia na Kenneth Asamoah aliwainua mashabiki wa Yanga kwa kufunga bao dakika ya 73 baada ya kupata pasi ndefu kutoka katikati ya uwanja na kumchambua kipa, Deogratius Munishi.

Yanga kama iliamka usingizi baada ya kufunga bao hilo ambapo dakika saba baadaye, ilizidisha mashambulizi na katika harakati za kuokoa beki wa Mtibwa, Salvatory Ntebe alijikuta akitumbukiza mpiwa wavuni kutokana na krosi ya Hamis Kiiza.

Baada ya kufunga mabao hayo, Yanga ilitulia na kuanza kupiga pasi nyingi huku wakicheza kwa kujiamini ambapo na kuwafanya Mtibwa kuusaka mpira.

Lakini dakika 86 ilifanya shambulizi la kushutukiza na Shamte Ally aliyeingia badala ya Godfrey Taifa aliifungia timu yake bao la tatu baada ya kupiga krosi iliyotinga moja kwa moja wavuni.

Yanga ikiwa imeshajihakikishia ushindi huo, dakika ya 90, Mtibwa ilifunga bao la kufutia machozi kupitia kwa Said Rashid aliyetumia vema uzembe wa mabeki wa Yanga waliozembea kuondosha hatari.

Akizungumzia mchezo huyo Kocha wa Mtibwa, Tom Olaba alilaumu uamuzi kutokuwa mzuri huku akisema Yanga ilibebwa ambapo katika mechi ya Zamaleki itawaumbua.

Yanga: Shaaban Kado, Godfrey Taita/Shamte, Stephano Mwasika,  Nadir Haroub 'Canavaro', Athuman Idd, Salum Telela/Juma Seif 'Kijiko', Omega Seme, Haruna Niyonzima, Davies Mwape, Kenneth Asamoah na Hamis Kiiza.

No comments:

Post a Comment