09 February 2012

Simba: Azam kwanza, Kiyovu itafuata

Na Zahoro Mlanzi

VINARA wa Ligi Kuu Bara, timu ya Simba imesema kwa sasa nguvu zao wanazielekeza katika mechi yao ya Jumamosi dhidi ya Azam FC itakayopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na baada ya hapo ndipo wataigeukia Kiyovu ya Rwanda.

Simba itakutana na Azam siku hiyo katika mfululizo wa mechi za ligi hiyo katika mchezo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na matokeo ya hivi karibuni zilipokutana.

Baada ya mechi hiyo, Simba inakabiliwa na mchezo wa awali wa Kombe la Shirikisho ambapo inatakiwa isafiri mpaka jijini Kigali katika mechi itakayopigwa kati ya Februari 17, 18 1u 19 mwaka huu.

Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya timu hiyo, Ibrahim Masoud 'Maestro', alisema kwa sasa akili zao na nguvu wanazielekeza kwa Azam na si sehemu nyingine.

"Unajua Jumamosi tuna mechi ngumu dhidi ya Azam, hivyo hakuna tunachofikiria kwa sasa zaidi ya mechi hiyo na lengo letu ni kuibuka na ushindi ili tujiimarishe katika mbio za kutwaa ubingwa," alisema Maestro.

Alisema kwa sasa hawataeleweka endapo wakianza kuzungumzia mechi dhidi ya Kiyovu wakati mechi iliyopo mbele yao ni ngumu na inavuta hisia za mashabiki wengi wa timu hiyo.

Mbali na hilo, pia alipoulizwa kuhusu maendeleo ya majeruhi mshambuliaji Felix Sunzu ambaye alianza mazoezi mepesi pamoja na Ulimboka Mwakingwe, alisema kwa wakati huo (jana) hakuwa na taarifa zaidi ya wachezaji hao tofauti na zilizotolewa awali.

Simba kwa sasa wanaongoza ligi hiyo wakiwa na pointi 34 (kabla ya mechi ya Yanga na Mtibwa Sugar ya jana), ikifuatiwa na Azam yenye pointi 32 na Yanga ipo nafasi ya tatu kwa pointi 31.

No comments:

Post a Comment