03 February 2012

Waziri Sitta aanika ugonjwa wa Mwakyembe

Ni katika ibada iliyofanyika kwa Mchungaji Gwajima
*Asema ponaji yake ni sumu kutoingia moyoni, figo
*Dkt. Mwakyembe naye asimama atoa ushuhuda wake
*Lowassa achangisha mamilioni ya fedha kanisani



Na Anneth Kagenda

KUNDI la wanasiasa maarufu kama waliojipambanua, kupambana na ufisadi ndani ya Serikali ya CCM,  wakiwemo Waziri  wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Dkt. Harrison Mwakyembe, wametoa ushuhuda uliosisimua umati wa watu kwenye ibada iliyofanyika katika Kanisa la Ufufuo na Uzima.

Ibada hiyo iliyofanyika Dar es Salaam jana, iliongozwa  na Mchungaji Kiongozi, Bw. Josephat Gwajima, kwa ajili ya Uzinduzi wa Programu ya Neno la Hekima kwa Kiongozi.

Waumini waliohudhuria ibada hiyo kwa mara ya kwanza walimshuhudia kwa karibu, Dkt. Mwakyembe, ambaye kwa siku za karibuni alikuwa nchini India kwa matibabu, ambapo pia alipewa fursa ya kusalimia waumini hao.

Ingawa ugonjwa wa Dkt. Mwakyembe umeendelea kuwa siri, hasa kwa viongozi wa serikali,  kwa mara nyingine, Bw. Sitta, alitumia fursa hiyo ya ibada kuwaambia waumini hao kuwa waziri (Dkt.Mwakyembe) alipewa sumu.

"Kwanza ninamshukuru Mungu kwa kumponya Dkt. Mwakyembe, na wale wote waliohusika katika hili watakiri na kuamini kwamba Mungu si wa mchezo, na mimi ninakiri hadharani kuwa alipewa sumu, lakini Mungu kamponya," alisema Bw. Sitta na kuongeza;

"Waliohusika wajue kuwa hawawezi kupambana na nguvu ya Mungu, kwani mkono wake ni mrefu kuliko kitu chochote."

Bw. Sitta alizidi kusisitiza kuwa; "Kama Dkt. Mwakyembe hakupewa sumu, basi vyombo vinavyofanya uchunguzi vitwambie haraka ilikuaje mpaka akafikia hali hiyo."

Alisema kuna watu wanapenda madaraka makubwa na kusahau taifa lao na Watanzania kwa ujumla. "Lakini hawa waliokuwa wanamchezea waziri sasa imekula kwao," alisema, Bw. Sitta na kupokewa na vigelegele vya Bw. asifiwe, huku wengine wakisema; "Shetani ashindwe kwa jina la Yesu."

Alisema Dkt. Mwakyembe kupewa sumu kulitokana na baadhi ya viongozi wenye uchu wa madaraka ambao walitaka kummaliza kabisa.

Hata hivyo alisema kama Mungu hajapanga ya binadamu  hayawezi kutimia.  Bw. Sitta alisema pamoja na Dkt. Mwakyembe kubadilika ngozi hadi kufikia ngozi ya nne, aliyonayo sasa wabaya hao walidhani atakufa, lakini hilo halikuwezekana kutokana na maombi ya madhehebu mbalimbali.

"Nilienda hospitali aliyolazwa, nilishindwa kuamini kile nilichokiona Dokta (Mwakyembe) ngozi yake ilikuwa kama ya tembo, wakati miguu utadhani aliugua matende, na pale mfanyakazi wa hospitali alipofagia ni kama alikuwa akifagia unga," alisema Bw. Sitta na kuongeza;

"Tuliambiwa kuwa sumu aliyokula haikuingia kwenye moyo, figo wala maini, bali ilitoka nje ndio maana madhara haya yakajitokeza... halafu leo mtu anasema hakunywa sumu? Ni kitu ambacho hakiwezekani, sumu hiyo ingeingia kwenye moyo, figo na maini sasa angekuwa marehemu."

Alisema kutokana na haya yote yanayoendelea kutokea, wataendelea kuomba ili ifike siku wala rushwa wajulikana.

Bw. Sitta alisema kuna viongozi wanaotakiwa kuombewa zaidi kwa Mungu kutokana na kutumia uongozi na madaraka yao vibaya kuibia taifa huku wakiacha Watanzania wasijue la kufanya.

Kwa upande wake Dkt. Mwakyembe, akitoa neno la shukrani alisema; " Ni kweli Mungu kaniponya na ninawaomba muendelee kumuombea Mwandosya (Prof Mark) aliyeko India," alisema.

Naye Mchungaji Gwajima, alisema lengo mahususi la kuzindua program hiyo ni kutokana na kuwapo changamoto nyingi hasa zile za kisiasa, kiuchumi na kijamii tangu kupatikana kwa  Uhuru wake mwaka 1961.

"Serikali inayoshika hatamu imetoa uhuru wa kuabudu, licha ya taifa kuwa na madhehebu mengi na makabila mengi, hili ni jambo jema zuri na la kujivunjia, hivyo kama kanisa tunamshukuru Mungu kwa hilo," alisema Mchungaji Gwajima.

Viongozi wengine waliohudhuria ibada hiyo ni Mbunge wa Same Mashariki Bi. Anne Kilango, Mbunge Viti Maalum Mbeya Bi. Hilda Mgoe, Mbunge wa Mbeya Bw. James Lembeli, aliyekuwa Mbunge wa Vunjo, Bw. Aloyce Kimaro.

Wakati huo huo,  Suleiman Abeid, anaripoti kutoka Shinyanga kuwa Waziri Mkuu Mstaafu, Bw. Edward Lowassa, amewataka waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Shinyanga kuhakikisha wanachagua viongozi wachapa kazi watakaoweza kuiongoza vyema Dayosisi mpya ya Shinyanga inayotarajiwa kuundwa hivi karibuni.

Bw. Lowassa alitoa mwito huo jana mjini Shinyanga, alipokuwa akiongoza harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa la KKKT, Usharika wa Shinyanga Mjini, ambapo kiasi cha sh. milioni 114 zilihitajika ili kukamilisha ujenzi huo, ambapo walifanikiwa  kuvukwa lengo hilo, baada ya kuchangisha kiasi cha sh. milioni 204.

Alisema iwapo waumini wa kanisa hilo watafanya makosa katika kumchagua kiongozi mwenye sifa itakuwa kazi ngumu kuliongoza kanisa hilo vizuri.

1 comment:

  1. Wateule kuweni macho,kupokea pesa za mafisadi kama michango ya ujenzi wa kanisa na kadhalika ni sawa na kushiriki kwenye ufisadi.

    ReplyDelete