03 February 2012

Balaa la mgomo



Wagonjwa Muhimbili
watua kwa sangoma

*BAWATA latoa mwongozo wa kutoa tiba kwa wagonjwa
*Wasema kipindupindu, TB, kifafa cha mimba hapana
*Vitanda vyabaki vyeupe, waliobaki wakata tamaa
*Mbatia ashuhudia hali ilivyo mbaya, atokwa chozi


Grace Ndossa na Rehema Maigala

HUDUMA katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MHN) na Amana, zimezidi kuwa mbaya, huku idadi ya wagonjwa wakiwa wamezikimbia na kwenda kutibiwa kwa waganga wajadi maarufu kama Sangoma.

Gazeti hili lilitembelea Wodi ya Kibasila, Siwahaji na Mwaisela na kushuhudia vitanda vingi vikiwa havina wagonjwa, tofauti na awali ambapo walikuwa wakilala mzungu wanne vitandane na wengine uvunguni. Habari za kuaminika zilieleza kuwa wagonjwa wengi kwa sasa wanaenda kupata tiba kwa waganga hao.

Tofauti na siku za nyuma katika hospitali ya Muhimbili kuna ya ya utulivu ambao haujazoeleka kwa miaka mingi, hata ule muda wa kwenda kuona wagonjwa ukifika hali inaendelea vile vile.

Kwa lugha nyepesi ni rahisi mtu kuamini kuwa wagonjwa waliobaki hospitali hapo ni wale ambao hawana uwezo wa kuhamishiwa hospitali zingine.

Wagonjwa waliozungumza na gazeti hili walisisitiza kuwa huduma bado hazipo. Mhudumu wa chumba cha kuhifadhi maiti hospitalini hapo, alidhibitisha idadi ya vifo kuongezeka tofauti na miaka ya nyuma tangu alipoanza kufanyakazi kwenye kitengo hicho.

"Idadi ya watu waliokuwa wakifa kwa siku ni kubwa, sijawahi kuona hali hii," alisema na kuongeza; "Hata maiti zilizokuwa zikiletwa kutoka hospitali zingine nazo zilikuwa nyingine, kwa kweli nimeona umuhimu wa madaktari."

Mmoja wa wagonjwa aliliambia gazeti hili kuwa amekaa  wiki mbili hospitalini hapo akisubiri kufanyiwa upasuaji, lakini hajapata huduma hiyo hadi sasa.

Alisema alipofika kwenye chumba cha upasuaji, aliambiwa warudi kwani madaktrai hawapo.

Naye Meneja wa  Kitengo cha Dharura, Dkt. Silanda Optatus, alisema  hali bado si nzuri, kwani  wagonjwa wanafika wachache tofauti na siku za nyuma.

Alisema kitendo hicho kilikuwa kinapokea wagonjwa 80 hadi 100 kwa siku, lakini kwa sasa wanaopelekwa  ni 25.

Naye  Mwenyekiti wa Chama cha NCCR Mageuzi Bw. Jemes Mbatia, akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea  Hospitali za Amana na Muhimbili, alisema hali ni mbaya, hivyo Serikali inatakiwa kukaa meza  kutatua mgogoro huo .

Alisema mgogoro huo ukiendelea unaweza kuiondoa Serikali madarakani 2015, kwani si  sikivu kwa wananchi wake.

"Mwaka 1992 ulitokea mgomo kama huu hospitalini hapa, wakati rais akiwa Mzee Ali Hassani Mwinyi, walitumia busara  na kukaa pamoja na madaktari na kumaliza mgogoro huo," alisema Bw. Mbatia.

Alisema serikali inatakiwa kutumia hekima na busara zilizotumika kipindi cha nyuma kukaa nao ili kumaliza mgomo huo.

Pia alisema serikali ikubali haina madaktari wa kutosha katika sekta mbalimbali, hivyo ni vyema wakatumia busara kukaa nao ili upatikane muafaka.

Alisema vifo vinavyotokea katika kipindi hiki cha mgomo ni wazi kuwa serikali haiwezi kufikia malengo ya Millenia ya kupunguza vifo ifikapo mwaka 2015.

Naye Rachel Balama, anaripoti kuwa waganga wa tiba za jadi wameshauriwa kutoa tiba kwa magonjwa wanayoweza, hasa katika kipindi hiki wanachopokea wagonjwa wengi wanaokimbia hospitalini kutokana na mgomo wa madaktari.

Taarifa iliyotolewa  kwa vyombo vya habari na Mwenyekiti Taifa wa Baraza la Waganga Watafiti wa Tiba Asilia(BAWATA), Bw. Shaka Shemuiwa, ilieleza kuwa wagonjwa wengi kwa sasa wanaenda kwa waganga wa jadi, hivyo alishauri kama magonjwa wanayougua hawawezi kuyatibu wawashauri waende hospitali binafsi.

Aliwataka waganga hao wa jadi  kutoa tiba kwa magonjwa kama malaria sugu, kisukari, shinikizo la damu na maradhi ya akina mama.

Aliwataka waganga hao wasithubutu kutibu kipindupindu, kifua kikuu, kifafa cha mimba na mengineyo.

Wakati huo huo  madaktari wameombwa kaonesha uzalendo kwa kurejea kazini ili kuokoa maisha ya watu wanaokufa.

Mwito huo  umetolewa Dar es Salaama jana na Rais wa Mtandao wa Wanataaluma Tanzania (TPN) Bw. Phares Magesa, wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Bw. Magesa, pia aliitaka serikali iharakishe mazungumzo na madaktari na itoe ahadi ya kutekeleza madai yao kadri uwezo utakavyoruhusu.


Naye Tumaini Maduhu, anaripoti kuwa hali ya utoaji huduma katika Hospitali ya Amana, imeendelea vizuri, ingawa kuna manung'uniko ya hapa na pale.

Mmoja wa wagonjwa Bw Said Hassan, alisema huduma za matibabu zinaendelea vizuri tofauti na ilivyokuwa hapo awali.


No comments:

Post a Comment