Na Mwajuma Juma, Forodhani
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeombwa kuandaa sheria ambayo itaweza kuwadhibiti watu ambao wamekuwa wakiiba vitu vya asili katika majengo ya Mji Mkongwe na kuviuza nje ya nchi.
Ombi hilo lilitolewa mwishoni mwa wiki na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Urithi wa Mji Mkongwe, Bw.Mohammed Juma Mugheiry wakati akizungumza na Majira ofisini kwake Forodhani mjini Zanzibar.
Bw.Mugheiry alisema, jumuiya yake imekuwa ikikabiliwa na changamoto nyingi katika mambo mbalimbali ikiwemo wizi wa vitu hivyo vya asili ambapo wanashindwa kukabiliana nao kutokana na kutokuwepo sheria ya kwabana watu hao.
Alisema, hali hiyo imekuwa ikichangiwa kwa kiasi kikubwa na wananchi kutokana na kutoelewa thamani ya vitu hivyo pamoja na kutokuwepo sheria ya kuwabana.
Mwenyekiti huyo alisema, katika hifadhi ya mji huo ni lazima kuwepo sheria ili kuulinda mji huo.
“Changamoto kubwa katika jumuiya yetu ni umaskini, ambapo tunapata tatizo kubwa la fedha katika kuendeleza jumuiya yetu, pamoja na wizi uliokithiri wa mali asili katika majumba hayo," alisema.
Hata hivyo alisema kuwa pamoja na kuwepo kwa sheria lakini zinaonekana hazifanyi kazi, kutokana na kuwa watu hao wamekuwa wakionekana kufanya biashara kwa kutumia mali hizo na kuwauzia wageni.
Alisema, kufanya hivyo kumekuwa kukiwakosesha mapato makubwa Serikali, kwani wageni hao huweza kununua vitu hivyo kwa bei ya chini.
“Kutokana na hali hiyo, kuna haja ya kuwekwa sheria itakayowabana wale ambao wanaonunuwa na wanaouziwa ili kukomesha vitendo hivyo, kwani tukifanyika hivyo kutawakatisha tamaa wezi na wanunuzi," alisema.
Mbali na chanagmoto hizo pia, Bw.Mugheiry alisema kwamba, jumuiya yao imeweza kuwa na mafanikio makubwa ikiwemo kutoa mafunzo kwa mafundi, kutoa elimu juu ya uhifadhi wa mji huo pamoja na kuyanusuru baadhi ya majengo ambayo yalikuwa yamo mbioni kuharibiwa.
No comments:
Post a Comment