13 February 2012

Watuhumiwa kuchakachua fedha za miradi Kilindi

Na Yusuph Mussa, Kilindi

MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi, wameazimia kuwafikisha mahakamani wakuu wa idara 11 pamoja na vitengo vyake kwa madai ya ubadhirifu wa fedha kwenye idara zao ikiwemo ujenzi wa jengo jipya la halmashauri.

Madiwani hao walipitisha uamuzi huo baada ya kujadili kama Kamati ya Fedha taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na wao kuridhia, baada ya CAG kuonesha kuna ubadhirifu wa fedha uliofanyika kati ya mwaka 2008 na 2010.

Akisoma maamuzi hayo Diwani wa Kata ta Tunguri, Bw.Michael Bomphe aliwataja viongozi wote ambao watachukuliwa hatua za kisheria, kinidhamu na wale ambao watatakiwa kurejesha fedha zilizoibwa.

Bw.Bomphe alisema, uchunguzi wa CAG umeonesha maeneo saba yalifanyiwa ubadhirifu wa fedha ikiwemo ujenzi wa jengo la ofisi ya halmashauri.

Maeneo mengine ni ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji, miradi ya mfuko wa barabara, miradi ya idara ya kilimo ikiwa ni pamoja na ununuzi wa power tillers, miradi ya idara ya afya, miradi ya maji na utawala na mishahara.

Bw.Bomphe alisema, ukaguzi wa CAG umeonesha kuna ongezeko la sh.bilioni 1.3 kwenye ujenzi wa ofisi hiyo ambapo awali jengo hilo lilitakiwa kujengwa kwa sh.bilioni 1.5.

Pia lililkuwa likamilike ndani ya wiki 40, lakini limechukua zaidi ya wiki 157.

Alisema, baadhi ya 'madudu' yaliyobainika na CAG ni malipo ya vifaa yaliyofanywa kinyume cha Sheria ya Manunuzi ya mwaka 2004, sh. milioni 835.3, mradi wa power tillers kuchakachuliwa sh.milioni 40.

Halmashauri ilinunua trekta mbili kwa sh.milioni 70, lakini zikawekwa namba za watu binafsi T 682 BGW lililogawiwa kituo cha Kibirashi na trekta T 696 BGW kupelekwa kituo cha Mtoro pamoja na mafuta ya sh.milioni 6.2 ambayo matumizi yake hayajulikani.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga ambaye alialikwa kwenye baraza hilo, Luteni Mstaafu Chiku Gallawa aliusifu ujasiri wa madiwani katika kufichua 'uozo' na kusema anaungana na Rais Kikwete kuwa mchwa wamejaa kwenye halmashauri.

"Nawapongeza madiwani kwa kuingia kwenye vita hii. Na huu ndiyo uwakilishi... mimi ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama (Mkoa), pia natakiwa kuona rasimali za wananchi zinatunzwa," alisema.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Bw. Mussa Semdoe alisema waliona halmashauri yao imekuwa kama 'shamba la bibi' wakaamua kulifanyia kazi kwa kukaa Baraza la Madiwani, Aprili 13, mwaka jana na kuomba Ofisi ya CAG kuichunguza halmashauri hiyo

3 comments:

  1. Wataishia kuwafikisha mahakamani kama ilivyotokea kwa Bgamoyo. Tangu mwaka 2010 hadi leo hakuna kinachoendelea. Pinda aliishia kuwavua madaraka kama alivyofanya kwa Brandi Nyoni na Mtasiwa wa Afya.

    ReplyDelete
  2. Kuhusu bagamoyo hivi ni kweli tangu mwaka juzi hakuna aliyehukuimiwa? Inatisha. Tazizo liko wapi? Ni mahakama gani hiyo isiyo na uchungu na hao mchwa?

    ReplyDelete
  3. Kama ni kweli basi hiyo ni Bwagamoyo na nji imebwaga moyo. Serikali vipi?

    ReplyDelete