Na Mwajuma Juma, Bwawani
WAZIRI wa Katiba na Sheria Zanzibar, Bw.Abubakar Khamis Bakar amekiri kuwepo kwa mapungufu na matatizo katika utendaji kazi ndani ya wizara yake ikiwemo rushwa, mambo ambayo wanajaribu kuyatatua ili kufikia lengo la wizara kutekeleza mpango wa mageuzi.
Hayo aliyasema mwishoni mwa wiki Mji wa Bwawani kisiwani Unguja wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu sera, mipango na mikakati ya utekelezaji ndani ya wizara.
Alisema, rushwa imehamia kila upande katika utendaji wao, wakazi, serikalini, lakini wanajitahidi ili kuhakikisha kuwa suala hilo katika maeneo yao ya kazi linapigwa vita kwa nguvu.
Hata hivyo alisema, mbali na suala la rushwa pia katika mahakama kuna matatizo kadhaa ikiwemo upungufu wa majengo, vifaa vya kutendea kazi, uhaba wa mahakimu jambo ambalo linachangia kwa kiasi kikubwa kuzorotesha shughuli za watendaji katika mahakama.
Alisema, wizara yake imetoa mafunzo mbalimbali kwa watendaji wa mahakama kwa lengo la kutaka wananchi waridhike katika utendaji wa utoaji haki ndani ya mahakama.
Sambamba na hilo alisema, baadhi ya sheria katika wizara yake zinapaswa kufanyiwa marekebisho kwa kuwa baadhi yake zimepitwa na wakati.
Alisema, wakati wa kufanya marekebisho hayo ni vyema wakapata ushirikino kutoka kwa wanasheria na wananchi ili waweze kuijengea nguvu wizara.
“Nikweli kuna sheria za tangu mwaka 1960 na 1980 ambazo zote hizi, ni za muda mrefu hivyo zinahitaji kufanyiwa marekebisho, hili si kwa watendaji wa wizara tu bali ni kwa wananchi wote,” alisema.
No comments:
Post a Comment