13 February 2012

Kesi ya kikatiba yasajiliwa kortini

Na Daud Magesa, Mwanza

KESI ya Kikatiba iliyofunguliwa na Wakili wa Kujitegemea na mmoja wa wakurugenzi wa Kampuni ya Kabonde & Magoiga Advocates ya jijini Mwanza, Bw.Stephen Magoiga imesajiliwa juzi katika Mahakama ya Katiba Mwanza.


Shauri hilo namba moja la mwaka 2012 lilifunguliwa Januari 6, mwaka huu katika mahakama hiyo, ambapo walalamikiwa ni wanasheria wa Serikali ya Tanzania na Mapinduzi Zanzibar.

Wanasheria hao kwa pamoja wanashitakiwa kwa kushindwa kuchukua hatua na kufumbia macho baadhi ya vifungu vinavyokinzana na Katiba ya Jamhuri kutokana na mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Akizungumza kwa simu na mwandishi wa habari hizi, Msajili wa Mahakama Kuu Mwanza, Bw.Isaya Arufan alikiri kusajiliwa kwa kesi ambayo inatarajiwa kuwa kivutio mara itakapoanza kusikilizwa.

“Ni kweli kesi hiyo imesajiliwa tayari,hivyo kinachosubiriwa ni tarehe ya kutajwa, lakini sina uhakika itatajwa lini, ukizingatia kuwa imesajiliwa Februari 9 mwaka huu,” alisema Msajili huyo.

Hata hivyo kesi hiyo ilichelewa kusajiliwa baada ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Mwanza, kuwa likizo nje ya kituo cha kazi.

Kwa mujibu wa sheria, baada ya kufunguliwa kwa kesi hiyo Rais atajulishwa kuwepo kwa shauri hilo ambapo atapaswa kuteua majaji wenye uwezo wa kusikiliza kesi hiyo kwa idadi sawa kutoka pande zote mbili.

1 comment:

  1. Katika mchakato wa kuandika katiba mpya nadhani tuwaache wazanzibari waamue kama wanataka kuendelea kuwa katika muuungano au la. Wasiwasi wangu ni kuwa kama tutawaendekeza hawa wazanzibari tutajikuta tunapoteza muda mwingi wa kukabiliana na changamoto za maendeleo kujadili muungano.

    Wanachotaka ni kuwa Jamuhuri na si pungufu ya hilo!

    ReplyDelete