15 February 2012

Washauriwa kuwekeza hisa Benki ya MUCOBA

Na Eliasa Ally, Iringa

MKUU wa Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa, Bw. Evarista Kalalu amewataka wananchi katika wilaya hiyo kuacha tabia ya kutunza pesa ndani ya nyumba zao wanazokaa na badala yake wawekeza katika Benki yao ya Mufindi (MUCOBA) ili zitunzwe katika mazingira mazuri.

Mwito huo aliutoa jana wakati akizungumza na watendaji wa kata, vijiji na wananchi, katika mkutano uliofanyika mjini Mafinga, ambao uliitishwa na Benki ya MUCOBA ili kuwajengea uelewa walengwa hao ambao ni wananchi, maofisa mbalimbali namna ya kuwekeza katika benki hiyo.

Aisema, wananchi wengi bado hawajapata elimu na uelewa wa umuhimu wa kuweka na kutunza pesa benki, hali ambayo inawafanya wazitunze pesa zao kwa kuzichimbia chini na kuzificha uamuzi ambao ni hatari kwa kuwa amna usalama wa fedha hizo.

Bw.Kalalu alisema, MUCOBA kwa sasa imejitanua hususani katika maeneo ya vijijini hali ambayo wananchi wanatakiwa kutumia fursa hiyo kujinufaisha kwa kununua hisa, kuweka pesa na kupata mikopo mbalimbali ili waweze kuendelea zaidi kiuchumi.

Aliongeza kuwa MUCOBA ambayo makao makuu yake yapo Mufindi, mjini Mafinga kwa sasa imefungua ofisi ndogo za kibenki katika Tarafa ya Igowole ili kuwakaribia wananchi ambao walikuwa wanafuata huduma za benki hiyo hadi mjini Mafinga hali ambayo inaonesha mafanikio ya kuwafikia wananchi.

Awali Meneja wa Benki ya MUCOBA, Bw.Danny Mpogole akizungumzia hali ya maendeleo ya benki hiyo alisema, inakabiliwa na matatizo kadhaa yakiwemo ya uelewa mdogo wa wananchi hususani wa maeneo ya vijijini kuwa pesa zao endapo
zitawekwa benki zitakuwa salama.

Hata hivyo alisema, kwa sasa benki hiyo pia inakabiliwa na mtaji mdogo, watu ambao wanakopa pesa kushindwa kuzirejesha kwa wakati na kushindwa kuwafikia kwa wakati mwafaka wananchi wengine ambao wanaishi maeneo ya vijijini kutokana na kuwepo kwa upungufu wa vitendea kazi.

Bw.Mpogole aliongeza kuwa ili kuhahakikisha kuwa huduma za kibenki zinakua
na kuwafikia wananchi wengi zaidi MUCOBA imejipanga kupanua huduma zake
vijijini ili kusogea karibu na wananchi.

Alisema, hadi sasa benki inajenga ofisi katika Kijiji cha Igowole na itaendelea katika kata nyingine wilayani humo.

Pia alisema kuwa MUCOBA inajipanga kuimarisha utumiaji wa fedha kwa kutumia
mitandao ya simu za mikononi, kuanzisha huduma za ATM ili kupunguza misongamano katika tawi lililopo mjini Mafinga na kuwezesha
wananchi wengi kunufaika.

Alisema, benki hiyo tayari imejiunga na huduma za Western Union Money Transfer hali inayowawezesha kukopa pesa kutoka pande zote za Dunia.

Hata hivyo alitoa mwito kwa wananchi kununua hisa za benki hiyo ambapo kila hisa inauzwa kwa sh. 500 na wananchi kwa kununua hisa za benki hiyo watakuwa na fursa kubwa ya kukopa pesa nyingi ili kuendeleza miradi yao.

No comments:

Post a Comment